UONGOZI wa Yanga SC umeweka wazi kuwa kwa sasa haupo tayari kupokea pigo jingine kwenye mechi zijazo za ushindani mara baada yakupoteza mchezo wa Kariakoo Dabi.
Oktoba 10,2026 ubao wa Uwanja wa Uhuru ulisoma Simba SC 2-1 Yanga SC. Ali Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari Yanga SC amesema kwa sasa hawapo tayari kupata pigo jingine tena.
“Ndugu zangu wanayanga, binafsi sitamani kuona tukipata pigo jingine baada ya kupoteza Kariakoo Derby. Na naamini hakuna mwanachama au shabiki wa Yanga ambaye angependa kuona hali hiyo ikitokea.
“Kupoteza derby tayari kumetuumiza. Ikiwa tutashindwa pia kufuzu hatua inayofuata ya CAF Champions League, itakuwa ni pigo kubwa kwa klabu na mashabiki wetu.Kwa hiyo, ninawaomba sana wanachama na mashabiki wetu tuamke sasa na kuelekeza nguvu zetu katika mchezo huu muhimu.
“Kuanzia sasa, katika makundi yetu ya WhatsApp, kwenye mitandao ya kijamii na katika mazungumzo yetu ya kila siku, tuhamasishe timu yetu, tujenge morali na tuoneshe mshikamano.Tusiendelee kutumia nguvu zetu nyingi katika maumivu ya matokeo yaliyopita. Badala yake, tuyatumie maumivu hayo kama sababu ya kuongeza ari na dhamira ya kushinda mchezo unaofuata.
“Wachezaji wanahitaji kuona kwamba mashabiki wao bado wapo pamoja nao. Wanahitaji kuona imani, mshikamano na hamasa kutoka kwa wanachama na wapenzi wa klabu,” amesema Kamwe.