MASHABIKI wameibuka na malalamiko makubwa mitandaoni kufuatia Azam FC kutangaza viingilio vya mechi yao dhidi ya Simba SC itakayochezwa Jumapili, Aprili 5, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiingilio cha chini (mzunguko) kimewekwa Shilingi 15,000, huku VIP B ikiwa Shilingi 25,000 na VIP A pia ikiwa Shilingi 30,000.
Bei hizo zimezua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki, wengi wakieleza kushangazwa na kiwango hicho cha viingilio kwa mechi inayochezwa Chamazi, Mbagala, wakidai gharama za usafiri pia ni kubwa.
Baadhi ya mashabiki wamehoji sababu ya kupandishwa kwa viingilio hivyo, wakidai klabu hiyo haina changamoto ya kifedha kiasi cha kuweka bei kubwa kwa mashabiki wake.
Mchezo huo wa “Mzizima Derby” unatarajiwa kupigwa kesho majira ya saa moja usiku, ukiwa ni miongoni mwa mechi zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka nchini.
