Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka rekodi ya kipekee katika historia ya michezo nchini baada ya kufanikisha timu nne za Tanzania kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa barani Afrika.
Timu hizo ni Simba SC na Young Africans SC (Yanga) zilizopenya hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League), huku Azam FC na Singida Fountain Gate FC zikifuzu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Hatua hii imechukuliwa kama matunda ya juhudi na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya michezo chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ikiwemo mpango wa “Goli la Mama”, ambapo kila goli lililofungwa na timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa lilikuwa na zawadi ya Tsh milioni 5 kutoka kwake binafsi — hatua iliyoongeza hamasa kubwa kwa wachezaji na klabu.
Wadau wa michezo wamesifu uamuzi huo, wakisema umechangia kuleta ari mpya na kuipa Tanzania hadhi ya juu katika soka la Afrika.