Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limetangaza ongezeko la asilimia 45 ya pesa za zawadi kabla ya kuanza kwa kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON).
Morocco itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo kuanzia Julai 5-26 katika miji mitano tofauti.
Bingwa ataondoka na kitita cha USD1,000,000, ongezeko la 100%, huku mshindi wa pili akiweka mfukoni USD500,000. Hapo awali bingwa alikuwa anavuna USD500,000 na mshindi wa pili USD300,000.
Timu iliyoshika nafasi ya tatu sasa itachukua USD350,000, nafasi ya nne USD300,000, huku timu nne zilizotolewa kwenye hatua ya robo zikichukua USD200,000 kila moja. Timu zote zinazoshiriki shindano hilo zitaondoka na pesa taslimu kwani timu zilizoshika nafasi ya 3 katika kila kundi zitapata USD150,000 na za nne zitachukua dola 125,000.
Wenyeji Morocco wataanza kampeni kwa mechi ya Kundi A dhidi ya Zambia. Tanzania ndiyo timu pekee kutoka baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na kati (CECAFA) iliyofuzu WAFCON.