AL AHLY YATWAA TUZO TIMU YA MWAKA AFRIKA, DIAMOND ATOA SHOO

KWA mara ya pili mfululizo Klabu ya Al Ahly ya Misri ambao ni Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2024 imeshinda tuzo ya timu ya mwaka 2024 kwa ngazi ya klabu huku msanii kutoka Tanzania, Diamond akipiga bonge moja ya shoo.

Kwa upande wa Wanawake tuzo hiyo imekwenda kwa timu ya wanawake ya TP Mazembe huku timu bora ya mwaka kwa ngazi ya kimataifa kwa wanaume ni Ivory Coast na Nigeria ikishinda tuzo hiyo kwa upande wa Wanawake
Nyota wa Klabu ya Atalanta ya Italia na timu ya taifa ya Nigeria, Ademola Lookman ambaye ni mshambuliaji ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Shirikisho la soka Afrika (Ballon d’or) kwenye tuzo za CAF zilizofanyika Mjini Marrakesh , Morocco.
Lookman (27) amewashinda Simon Adingra wa Ivory Coast, Serhou Guirassy wa Guinea, Achraf Hakimi wa Morocco na Ronwen Williams wa Afrika Kusini.
Kocha wa timu ya Taifa ya lvory Coast, Emerse Fae ameshinda tuzo ya kocha bora wa mwaka 2024 wa Afrika akiwashinda kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini Hugo Broos na kocha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sebastien Desabre.

Fae (40) raia wa Ivory Coast aliiongoza timu hiyo kushinda taji la AFCON akiwa kama kocha wa muda, kabla ya kupewa ajira rasmi baadaye.