MWAMBA Djigui Diarra kipa namba moja wa Yanga msimu wa 2024/25 amekimbiza kwa kutimiza majukumu yake akiwa langoni kwa kuanza jumla ya mechi 9 kikosi cha kwanza.
Ikumbukwe kwamba Yanga ni mechi 10 wamecheza kwenye ligi na ushindi ni mechi 8 huku kichapo ikiwa ni kwenye mechi mbili ambazo zote alianza langoni Diarra.
Katika mechi hizo za kupoteza ilikuwa Yanga 0-1 Azam FC na Yanga 1-3 Tabora United zote zilichezwa Uwanja wa Azam Complex Yanga wakiwa nyumbani.
Zama hizo mpanga mipango alikuwa ni Miguel Gamondi ambaye amepewa mkono wa Thank You na sasa mikoba yake ipo mikononi mwa Sead Ramovic, raia wa Ujerumani ambaye mchezo wake wa kwanza unatarajiwa kuwa dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambao ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi moja ni Khomein alikaa langoni ilikuwa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union baada ya dakika 90 ubao ulisoma Coastal Union 0-1 Yanga bao la ushindi likifungwa na Jean Baleke ikiwa ni bao lake la kwanza ndani ya ligi.
Aboutwalib Mshery hajapata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza msimu wa 2024/25 na aliweka wazi kuwa kila mchezaji ana nafasi ya kucheza kulingana na mpango kazi wa kocha anayepanga kikosi.