UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa kocha mpya wa timu hiyo raia wa Ujerumani amekuja na aina mpya ya kucheza inayokwenda kwa jina la gusa achia twende kwao.
Ni Sead Ramovic huyu ni mrithi wa mikoba ya Miguel Gamondi ambaye kwenye Ligi Kuu Bara aliongoza kikosi kwenye mechi 10 msimu wa 2024/25, ushindi mechi 8 na aliambulia kichapo kwenye mechi mbili.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa kocha huyo anapenda shangwe kutoka kwa mashabiki hivyo wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa, Novemba 26 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambao ni hatua ya makundi.
“Siku ya Jumanne natamani kumuona Kila Mwananchi akiwa uwanjani kuwapa hamasa wachezaji wetu, safari hii tumepa mwalimu anayependa shangwe la mashabiki, ‘German Machine’ Ramovic anatamani kuwaona siku hiyo. Niwaombe tu Wananchi Wenzangu, tukate tiketi mapema tusisubiri siku ya mechi ifike
“Jumanne ni siku ambayo Tanzania yote itatulia na kuufatilia mchezo wetu dhidi ya Al Hilal, kocha wetu ‘German Machine’ Ramovic ametambulisha soka linaloitwa ‘GUSA ACHIA TWENDE KWAO’ baada ya kutazama hili Soka mazoezini nikaona kabisa Wananchi tunakwenda kupata raha siku ya Jumanne. Niwaombe msiwe watu wa kuikosa furaha hii.”