BENCHI la ufundi la Mashujaa limebainisha kuwa linahitaji pointi tatu za mnyama kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ya NBC unaotarajiwa kuchezwa leo Novemba Mosi 2024, Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma.
Huu ni mchezo wa kwanza kwa timu zote mbili ndani ya ligi kwa Novemba ambapo kila timu hesabu kubwa ni kusepa na pointi tatu mazima uwanjani.
Abdallah Bares, Kocha Mkuu wa Mashujaa amesema kuwa wanatarajia kuwa na mchezo wenye ushindani mkubwa kutokana na mwendelezo wa Simba kwenye mechi zao hivyo wamejipanga kupata matokeo mazuri.
“Mwendelezo wa Simba kwenye mechi zilizopita unaonekana ulikuwa bora ila nasi tumepata pointi moja mchezo uliopita hali inayotuongezea nguvu ya kujiamini hivyo tutaingia uwanjani kwa tahadhari na kutafuta ushindi.”
Mchezo uliopita kwa Mashujaa ilikuwa Oktoba 28 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Fountain Gate 2-2 Mashujaa huku Simba mchezo wao uliopita ilikuwa Simba 3-0 Namungo.