MANCHESTER UNITED IMEMTEUA AMORIM KUWA KOCHA MPYA

Manchester United wamemchagua kocha wa Sporting, Ruben Amorim kuwa meneja wao mpya.

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye atahamia Old Trafford kutoka klabu ya Lisbon mnamo Novemba 11, ametia saini mkataba hadi Juni 2027.

Mshambulizi wa zamani wa United Ruud van Nistelrooy, ambaye alichukua jukumu la kuinoa kwa muda baada ya Erik ten Hag kutimuliwa Jumatatu, atasalia kwa mechi tatu zijazo za klabu hiyo.

Amorim, ni meneja wa sita wa kudumu United kumchagua tangu utawala wa miaka 26 wa Sir Alex Ferguson kumalizika na kustaafu mwaka 2013.

Sporting ilithibitisha katika taarifa kwamba Manchester United wamekubali kulipa euro 11m (£9.25m) ili kuwezesha kuondoka kwake kama ilivyo katika mkataba wa Amorim.

Mechi ya kwanza ya Amorim huko Manchester United inatarajiwa kuwa Novemba 24, baada ya mapumziko ya kimataifa, kwenye Ligi ya Primia dhidi ya Ipswich iliyopanda daraja.