>

GAMONDI ATAJA TATIZO LA YANGA LILIPO

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa tatizo kubwa ambalo lilikuwa kwenye mchezo wao wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ni kushindwa kutumia nafasi ambazo walizipata ndani ya uwanja.

Ni Agosti 29 2024 ilikuwa Uwanja wa Kaitaba baada ya dakika 90 ulisoma Kagera Sugar 0-2 Yanga na mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 25, Clement Mzize dakika ya 88 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Gamondi amesema kuwa kilichotokea wanakwenda kukifanyia kazi ili kuwa bora kwenye mechi zinazofuata ikiwa ni pamoja na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya  CBE ya Ethiopia.

“Ulikua ni mchezo wenye ushindani mkubwa kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi zaidi ya sita lakini tukapata bao moja na ilikuwa hivyo kipindi cha pili tulipata nafasi tatu tukatumia moja, sio mbaya kwa hili lililotokea kikubwa ni pointi tatu na makosa haya tunakwenda kufanyia kazi eneo la mazoezi.

“Kuna mchezo wa Ligi ya Mabingwa utakuwa mgumu kwetu hasa ukizingatia kwamba kuna wachezaji ambao watakuwa kwenye timu ya taifa na watarejea muda mfupi, kuna kazi kubwa ambayo tunakwenda kufanya nina amini tutafanya maandalizi mazuri kwa muda ambao tutaupata.”