YANGA YATAMBIA KIKOSI BORA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa una timu bora kwa sasa kutokana na usajili bora waliofanya kwa wachezaji wazuri na kuhakikisha wachezaji wenye uwezo wapo ndani ya timu.

Ipo wazi kuwa Yanga msimu wa 2023/24 walitwaa taji la Ligi Kuu Bara, CRDB Federation Cup na iligotea hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amebainisha kuwa haikuwa kazi rahisi kuwapata wachezaji wenye uwezo mkubwa hilo lipo wazi na linaongeza thamani ya ligi ya Tanzania.

“Msimu huu hata msiposema mawe yatazungumza kwamba Yanga tuna timu bora kwa kuwa kuna wachezaji wazuri wenye ubora na hilo linafanyika kwa sasa kuwa imara kila eneo ndani ya uwanja.

“Kila Mwanayanga anafurahi kwa sasa kwa sababu kila eneo kuna wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa hili linatupa nguvu ya kuwa imara kwenye mashindano ambayo tutashiriki.”.

Usajili wa kwanza ndani ya Yanga ambao umeleta mtikisiko Bongo ni wa Clatous Chama ambaye ameibuka hapo bure akitokea Simba yeye ni kiungo mshambuliaji.

Saini ya Aziz Ki ambaye alitambulishwa Julai 10 kuwa bado ni Mwananchi ilizua gumzo barani Afrika kwa kuwa alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za timu mbalimbali.