>

DKT. ABBASI: MAPANGO YA AMBONI NI HAZINA KWA TAIFA YANATAKIWA KUTUNZWA

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema mapango ya kihistoria na yenye maumbo ya kipekee ya kijiografia ya Amboni, Tanga ni hazina ya Taifa na yanatakiwa kutunzwa ili vizazi vijavyo viweze kujionea historia kubwa inayopatikana katika eneo hilo.

Amesema hayo leo Julai 9, 2024 mara baada ya ziara ya kutembelea maeneo hayo yanayolindwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kuzungumza na wafanyakazi.

“Tutunze mapango haya na tuweke juhudi katika kuyatangaza ili tuweze kupata watalii wengi zaidi. Kama Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoka ofisini na kwenda kutangaza vivutio vya nchi yetu nasi hatuna budi kufanya hivyo”, alisema Dkt. Abbasi.

Mapango ya Amboni yamejaa historia kubwa ya nchi ikiwemo kutumika kama eneo la kujificha wapigania uhuru dhidi ya wakoloni, historia na kisa cha Otango Osale na wenzake katika kuwachezea shere wakoloni na pia kuna maumbo ya kipekee yanayosadifu vitu mbalimbali kama wanyama na maumbile mengine na mtu huweza kutembea ndani ya mapango hayo kwa kilometa kadhaa akijionea maajabu mbalimbali.