>

MSANII WA MUZIKI WA RAP KUTOKA MAREKANI, FATMAN SCOOP, AFARIKI BAADA YA KUANGUKA JUKWAANI

Msanii wa muziki wa Rap kutoka Marekani, Fatman Scoop, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 53 baada ya kuanguka kwenye tamasha lake siku ya Ijumaa huko Connecticut.

Alikuwa katikati ya tamasha hilo katika eneo la Town Centre Park kwenye mji wa Hamden pale alipoanguka jukwaani.

Meya wa eneo hilo, Lauren Garrett aliandika kupitia mtandao wa Facebook kuwa msanii huyo alipelekwa katika hospitali ya mtaa na gari la kubeba wagonjwa.

Lakini shirika lake lililokuwa linasimamia shughuli zake za mziki, MN2S, lilithibitisha kifo chake kupitia taarifa likisema kwamba “alama nzuri ya mzaliwa huyo wa New York itaendelea milele kupitia muziki wake”.

Scoop, ambaye jina lake rasmi ni Isaac Freeman III, ametambuliwa kama mtu mashuhuri katika eneo la muziki wa hip hop la New York City katika miaka ya 1990.

Ameshiriki kwenye nyimbo maarufu ikiwa ni pamoja na Lose Control iliyoshinda tuzo ya Grammy ya Missy Elliott na It’s Like That ya Mariah Carey.

Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, familia ya Scoop ilisema alikuwa “mtu mzuri sana, ambaye ni mfano bora kote jukwaani na katika maisha”