BILIONEA AMUITA CHAMA DAR FASTA

RAIS wa Heshima ambaye pia Mwekezaji wa Simba, Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ amebadili maamuzi na haraka amemuita kiungo wao mshambuliaji, Mzambia Clatous Chama Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo kuongeza mkataba mpya kuendelea kubakia hapo.

Awali ilielezwa kuwa Mo aliwagomea baadhi ya Viongozi wa Bodi ya Klabu hiyo kumuongezea mkataba kiungo huyo kutokana na kiwango kidogo ambacho amekionyesha katika msimu uliopita.

Kiungo huyo ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao imemalizika mwisho mwa msimu uliomalizika ambao Yanga wamebeba Makombe yote Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kiungo huyo huyo tayari yupo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha dili hilo la usajili Simba.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, kama mazungumzo yatakwenda vizuri kati ya Chama na Mo, katika dau la usajili na mshahara unakadiliwa kufikia zaidi ya Sh 40Mil, basi atasaini mkataba kabla ya kurejea nyumbani kwao.

Aliongeza kuwa kiungo huyo anaandaliwa mkataba wa miaka miwili wenye masharti kati ya hivo ni kuuvunja kama akishindwa kuonyesha kiwango bora katika msimu ujao.

“Chama yupo nchini ametua ndani ya hizi siku mbili akitokea kwao Zambia alikokwenda kwa ajili ya mapumziko na yupo hapa kwa ajili ya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na Mo ndiye aliyemuita.

“Mazungumzo hayo yatakwenda sambamba na kikao kizito kati yake ya Mo, lengo ni kuhakikisha wanamuongezea morali ya kuipambania timu ili msimu ujao warejeshe heshima ya klabu.

“Ninaamini mazungumzo yatakwenda vizuri kati ya Chama na Mo kwani yalishafanyika mazungumzo ya awali kabla ya kutua nchini hivyo upo uwezekano mkubwa wa kubakia hapa Simba,” alisema mtoa taarifa.

Akizungumzia hilo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa “Wanasimba waondoe hofu, usajili mkubwa unakufanywa na viongozi wetu, kikubwa tushikamano katika kipindi hichi kigumu.”

STORI NA WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI