YANGA YAFUNGUKIA AZIZ KI KUIBUKIA SIMBA

WAKATI jina la mfungaji bora ndani ya ligi msimu wa 2023/24 Aziz Ki kiungo mshambuliaji wa Yanga likitajwa kuwa kwenye hesabu za watani zao wa jadi Simba, bosi wa Yanga amefungukia ishu hiyo.

Ni mabao 21 Ki alifunga akitoa pasi 8 za mabao na alihusika kwenye mabao 29 ndani ya timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi raia wa Argentina.

Gamondi kaongezewa kandarasi ya mwaka mmoja huku Aziz Ki ambaye alikuwa ni chaguo la kwanza kwa kocha huyo bado hajaongeza mkataba mpya kuendelea na majukumu yake kwa msimu mpya kwa sasa ni mchezaji huru.

Inaelezwa kuwa kuna timu zaidi ya mbili ambazo zinahitaji saini yake ikiwa ni Simba ya Tanzania, Mamelod Sundowns na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini.

Kamwe amesema: “Kuna timu nyingi ambazo zinahitaji saini ya Aziz Ki tunalitambua ila kuhusu yeye kwenda kwa watani zetu wa jadi, (Simba) labda atakuwa ni Aziz mwingine ila sio huyu ambaye furaha yake ni ndani ya Yanga.

“Mazungumzo yanaendelea kuhusu mkataba wake mpya kwa kuwa kinachohitajika kinajulikana hivyo mashabiki wasiwe na presha, maisha ya mpira yana mengi hivyo taarifa zikikamilika tutaweka bayana kila kitu.”

Taarifa zinaeleza kuwa Aziz Ki amepewa dili la miaka miwili ndani ya Yanga kwa ajili ya kuendelea kutimiza majukumu yake kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.