AZAM FC KUFANYA KITU KIMATAIFA

UONGOZI wa Azam FC umebainisha kuwa kwenye anga la kimataifa wanaimani watafanya kitu kikubwa ambacho kitawashangaza wengi ambao hawana imani na timu hiyo.

Ipo wazi kwamba Azam FC itapeperusha bendera ya Tanzania kwenye anga la kimataifa baada ya kugotea nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa kila kitu kipo kwenye mpango bora na walikuwa wanahitaji kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tulianza msimu kwa mpango kazi kutokana na kile ambacho kilikuwa kwetu na wengi hawakutarajia kwamba tutakuwa hapa na imetokea kwa kuwa tunakwenda kimataifa tutafanya kitu.

“Mpango wa mwanzo ilikuwa kufanya vizuri kwenye ligi ya ndani imekuwa hivyo na sasa tunakwenda kwenye anga la kimataifa tutafanya vizuri kwa kuwa mipango ipo vizuri.”

Kutoka ndani ya Azam FC kinara wa utupiaji mabao ni mzawa Feisal Salum ambaye aligotea kwenye mabao 19 msimu wa 2023/24 ikiwa ni miongoni mwa nyota waliofunga hat trick mapema zaidi kwenye mchezo dhidi ya Tabora United.

Aliyeongoza kwa utupiaji ni Aziz Ki wa Yanga ambaye alifunga jumla ya mabao 21 na bao lake la 10 alifunga kwenye mchezo dhidi ya Tabora United ugenini wa pigo huru.