MASTAA wawili wanaofanya kazi kubwa kwenye kutimiza majukumu yao ndani ya uwanja katika mechi za Ligi Kuu Bara, Aziz KI na Feisal Salum wamefungukia hatma yao kuhusu kutwaa tuzo ya kiatu cha ufungaji bora.
Mei 25 wababe hao wawili kila mmoja atakuwa kazini kupambania nembo ya timu ambapo Yanga watakuwa na kibarua dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Mkapa na Azam FC watakuwa na kibarua dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Azam Complex.
Aziz KI wa Yanga mwenye mabao 17 alifunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji akiwa namba moja. Ipo wazi kuwa kafunga mabao 15 akitumia mguu wa kushoto na mabao mawili kwa mguu wa kulia ndani ya uwanja.
Anapambania tuzo ya ufungaji na Feisal wa Azam FC mwenye mabao 16 wote wakiwa wamebakiwa na michezo miwili ambazo ni dakika 180.
Aziz KI kuhusu tuzo hiyo amesema : “Sifikirii kuhusu tuzo ya ufungaji bora kwa sasa bali ni malengo ya kupata ushindi kwa timu ipo hivyo, nikipata nafasi nitafunga ama kutoa pasi kwa mchezaji kwani kikubwa nikuona kwamba tunapata matokeo mazuri.”
Fei Toto amesema: “Kuhusu kufunga hilo ni furaha kwangu namshukuru Mungu sifikirii kuhusu suala la tuzo ya ufungaji bora kwanza malengo ya timu ikitokea nikiwa mfungaji bora nitamshukuru Mungu.”