SIMBA HESABU KIMATAIFA KUONGEZA DOZI, AL AHLY KUTUA LEO

BENCHI la ufundi la Simba limebainisha kuwa litawaongezea dozi wachezaji wao kwenye uwanja wa mazoezi kuwa imara zaidi katika mechi wanazocheza ikiwa ni pamoja na safu ya ulinzi.

Ipo wazi kwamba ndani ya Ligi Kuu Bara, safu ya ulinzi ya Simba imekuwa na mwendo mbovu katika ulinzi ndani ya timu tatu zilizo kwenye tatu bora msimu wa 2023/24.

Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba amesema kuwa wanatambua makosa yalipo jambo linalowafanya wafanye kazi kwa umakini kuelekea kwenye mechi zijazo kwa kuwaongezea wachezaji wao dozi nyingine.

“Unaona kwenye mechi ambazo tunacheza tunapata ushindi na wakati mwingine tunawapa ruhusa wapinzani kutufunga huwa tunaongea na wachezaji na tutaongeza dozi nyingine kwenye uwanja wa mazoezi.

“Kikubwa ni kuwa makini kwa kuwa mchezo wa mpira ni mchezo wa makosa, kuelekea kwenye mechi zetu zijazo tuna imani tutakuwa imara hilo linawezekana kutokana na wachezaji kujituma na kutimiza majukumu yao kwa ushirikiano,”.

Kikosi cha Simba baada ya kucheza mechi 19 ndani ya ligi ni mabao 18 ukuta umeruhusu ikiwa namba moja kwa timu ambazo zimefungwa mabao mengi ndani ya tatu bora msimu wa 2023/24.

Mchezo ujao kwa Simba ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika itakuwa dhidi ya Al Ahly unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Machi 29 tayari wapinzani wao wameanza safari kuja Dar wanatarajiwa kutua leo.