Home Sports AZAM FC KWENYE HATUA NYINGINE TENA

AZAM FC KWENYE HATUA NYINGINE TENA

MATAJIRI wa Dar,Azam FC wameendeleza mwendo wa kupiga hatua zaidi kwaajili ya kuwa na wachezaji bora na kuendeleza kutoa ajira kwa Watanzania kupitia sekta ya michezo.

Taarifa ambayo imetolewa na Azam FC imeeleza namna hii: “Tumeingia makubaliano ya ushirikiano na vituo vya kulea vipaji (academies) nane za mikoa mbalimbali nchini.

“Vituo hivyo nane vitakuwa ni ‘AZAM FC CENTERS’, vikituwakilisha katika mikoa husika, vikiwa na jukumu la kutafuta vipaji vya wachezaji vijana wa Kitanzania, watakaokuja kujiunga na kituo chetu ‘Azam FC Academy’ kutokana na mahitaji ya timu yetu.

Baadhi ya vituo hivyo tulivyoanza navyo ni JK7Pro Football Center (Tanga), Tutes Hub Sports Center (Songea), Maendeleo Youth Sports Center (Mtwara), Kilwa Youth Sports Center (Lindi).

“Vingine ni Muleba Youth Sports Center (Kagera), Mwanga City Sports Center (Kigoma), Rungwe Youth Sports Center (Mbeya) na Korogwe Youth Soccer Center (Korogwe).

“Azam FC tutavipa kipaumbele vituo hivyo katika kuvuna vipaji vya vijana, pale tutakapokuwa na uhitaji wa wachezaji kwenye kituo chetu.

“Lakini sisi kama Azam FC tunaothamini vipaji vya vijana wadogo, tutaendelea na jukumu letu la kila mara la kuvuna vipaji popote pale nchini, tukiendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika juhudi zake za kukuza maendeleo ya michezo nchini.

“Tayari makubaliano kati ya vituo vyote hivyo na Azam FC yameingiwa kwa mikataba rasmi, zoezi lililosimamiwa kwa ukaribu na Vice Chairman, Omary Kuwe.

“Mara baada ya zoezi hilo kukamilika, hivi karibuni benchi letu la timu za vijana, litatembelea vituo hivyo (Azam FC Centers) kwa ajili ya kukutana na makocha wanaofundisha vijana hao, lengo likiwa ni kuwajenga zaidi na kuwapa vigezo vya aina ya wachezaji wanaowahitaji.

“Kwa kuanzia, tumeanza na vituo hivyo nane, lakini katika ramani yetu tumepanga kuifikia Tanzania nzima kwa kuwa na ‘Azam Centers’ katika mikoa yote nchini.

“Tunaamini kuwa kupitia programu hii, klabu yetu itaweza kuvuna vipaji bora vya vijana wa Kitanzania na kuviendeleza zaidi pale watakapofika kwenye kituo chetu ‘Azam FC Academy,”.

Previous articleAMETUPA JIWE GIZANI BOSI YANGA ISHU YA TIMU KUUZWA
Next articleYANGA KAZINI TENA LIGI KUU BARA