TIMU yenye vipaji vikubwa na uwekezaji imara ndani ya Ligi ya Wanawake Tanzania, Fountain Gate Princess inayotumia Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kwa mechi za nyumbani inaivutia kasi Simba Queens.
Ipo wazi kuwa mchezo wao uliopita wakiwa nyumbani walipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na kuziacha pointi tatu zikisepa mazima.
Mchezo wao unafoata ni dhidi ya Simba Queens unaotarajiwa kuchezwa Februari 2 2024 ambapo wapinzani wao hao walitoka kuambulia ushindi wa mabao 7-0 Alliance Girls, Uwanja wa AzamComplex.
Mratibu wa Fountain Gate Princess, Issa Liponda wengi wanamtambua kwa jina la Issa Mbuzi alisema kuwa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya mechi zao zote.
“Mchezo wetu ujao ni dhidi ya Simba Queens, tupo tayari kuwakabili wapinzani hao wachezaji wanapewa maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi nina amini tutapata matokeo mazuri,” alisema Mbuzi.