TAIFA STARS NA MATUMAINI AFCON

NYOTA wa timu ya taifa ya Tanzania, Simon Msuva amesema kuwa bado wana nafasi ya kufuzu hatua ya makundi kwenye Kombe la Mataifa Afrika, (AFCON) nchini Ivory Coast licha ya kete ya kwanza kutokuwa na matokeo mazuri kwa Tanzania.

Ipo wazi kwamba katika mchezo wa kwanza uliochezwa Januari 17 ilikuwa Morocco 3-0 Tanzania waliomtungua Aishi Manula aliyeanza langoni ni Ghanem Saiss dakika ya 29 kipindi cha kwanza huku mabao mawili yalifungwa ndani ya dakika mbili kupitia kwa Aziz Eddine dakika ya 76 na Youssef En-nesyn dakika ya 78.

Msuva amesema: “Haikuwa malengo yetu kupoteza, wachezaji tulijituma na tulikuwa tunacheza na timu imara hivyo kupoteza mchezo wetu haina maana kwamba imefika mwisho bado tuna mechi nyingine tunaamini tutafanya vizuri kufikia malengo yetu,”.

Katika mchezo huo kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ulinzi pia Novatus Mirosh alionyeshwa kadi mbili za njano hali iliyoplekea kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi dakika ya 70 kwenye mchezo huo.

Novatus baada ya mchezo aliweka wazi kuwa faulo ya pili iliyomsababishia kadi ya pili ya njano hakumchezea faulo mchezaji bali ilikuwa ni maamuzi ya mwamuzi mwenyewe pamoja na mchezaji mtego wake wa kumuhadaa mwamuzi kujibu.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu baada ya Stars kupoteza aliandika ujumbe huu kupita mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Instagram:” Mchezo mzuri usiku wa leo vijana wetu Taifa Stars japo bahati haikuwa upande wetu. Tunaendelea kuwatakia kila la kheri na Taifa liko nyuma yenu katika mechi zenu zinazofuata,”.

Mchezo unaofuata kwa Stars ni Januari 21 dhidi ya Zambia ambayo mchezo wake wa kundi F ilitoka kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 dhidi ya DR Congo.