CRIS JABAR MWAMBA ANAYEWAZA KITAIFA NA KIMATAIFA

UKIITAJA Tandale basi utapewa zile habari za mwamba Nassib Abdul ambaye jina lake maarufu anaitwa Diamond kuwa yeye hapo ndio maskani yake na muziki wake ulianzia hapo mpaka leo      katusua kitaifa na kimataifa.

Vipaji vingi vipo Nyanda za Juu Kusini pia ambapo ukiigusa mitaa ya Njombe Mjini mitaa ya Mpechi kuna Christopher Muhagama jina la kutafutia ugali ni Chris Jabari yeye anaibeba Njombe akiwa anawaza kutusua kitaifa na kimataifa pia.

Huyu hapa ambaye kafunguka mengi namna hii:-

Mwaka uliopita kipi ulifanikiwa?

“2023 ulikua ni mwaka niliopanga kuachia nyimbo mbili, lakini kutokana na mabadiliko ya mipango nikawa nimeachia wimbo mmoja tu unaoitwa Sina Mashaka ambao umenipa nafasi ya kunirudisha katika nafasi yangu. Nyanda za juu wamenipokea vizuri na unachezwa kwenye vituo mbalimbali.

 “Wimbo wapili niliokua nimepanga kuuachia mwaka 2023 nitauambatanisha katika EP yangu itakayoachiwa Januari mwisho mwa 2024 ama wa pili mwanzoni.

2024 mipango ipoje?

“Mpango wa 2024 ni kufanya jambo ambalo sikuwahi kulifanya kabla ambalo ni kuachia EP yenye nyimbo sisizopungua chini ya nne nazo ziende mbali zaidi ya nyimbo nilizowahi kuachia awali. Kuhusu albamu hesabu zipo labda kuanzia 2025 ndo ndo naweza nikaachia.

Kuhusu video Mungu ni mwema mambo yakikaa sawa tutaachia video pia mwaka huu kwa ajili ya wapenzi wa muziki na lengo kubwa ikiwa ni kuwa na mchango katika maendeleo ya burudani ya taifa letu.

Muziki umekupa nini?

“Muziki umenipa marafiki na ndugu wapya, kuaminika na watu ambao wengine hata sijawahi onana nao na jambo kubwa zaidi nimepata tumaini kwamba hata ikitokea nikaaga dunia leo bado nitakuwa naishi kwenye mioyo ya ya watu kwa kazi chache ambazo nimeziachia.

Kwa nini unafanya muziki?

Nafanya muziki kwa kuwa muziki hua unaambatana na mimi. Ingetokea ukawa karibu na mimi ungegundua huwa naimba mara kwa mara na mara nyingine hutokea hata bila mimi kuwa nimezingatia kuwa naimba au la.

“Kazi zangu naandika mwenyewe, ila mara chache inatokea kama kuna watu wengine studio napokuwa narekodi wakachangia baadhi ya maneno.

Najua Mungu ameweka kipaji ndani yangu basi nakubaliana na heshima ninayopewa ambayo mimi huwa naihesabia kama heshima na nilichokibeba, heshima ya Chris Jabari na sio heshima ya Christopher Mhagama. Njombe Mjini, Ludewa na Makete watu ni wako bize na shughuli zao mbalimbali za kulijenga taifa letu la Tanzania huku wakipata muziki mzuri.

Miaka mitano unajiona wapi?

“Kikubwa ni kuomba uhai na mengine yatafuata. Muziki wetu wa Njombe unazidi kukua taratibu na tunavuka mipaka tukipasua anga. Ushirikiano mkubwa kwa kila mmoja ni muhimu tunaona kabisa kuna mambo mazuri yanazidi kuja.

“Ndugu jamaa na marafiki wazidi kuendelea kuwa bega kwa bega nasi kwa kufuatilia kazi zetu ambazo zipo kwenye ukurasa wetu wa You Tube kuna nyimbo nyingi ikiwa ni pamoja na Mbali, Angalau hizi zote ni nzuri hivyo mengine yanakuja zaidi,” anamalizia Jabari.