>

SANKARA APIGA SIMU YANGA

MSHAMBULIAJI wa Asec Mimosas, Karamoko Sankara hatimaye amefunguka dili lake na Yanga huku akisema kuwa amekuwa akiwapigia simu wachezaji wa sasa wa Yanga, Pacome Zouzoua na Kouassi Attohoula Yao ambao ni marafiki zake.

Sankara amekuwa akihusishwa kwa muda sasa kutakiwa na Yanga huku msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amefanikiwa kufunga mabao 4 akiwa ndiye kinara wa michuano hiyo akifuatiwa na Pacome Zouzoua wa Yanga mwenye matatu.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Sankara alisema kuwa anafahamu na kuona tetesi za kuhitajika na timu nyingi hususani Yanga ambapo amesema kuwa hawezi kuweka wazi nini kinaendelea kwa sasa kwa kuwa yeye bado ni mchezaji wa Asec.

Aliongeza kuwa ndani ya Yanga amekuwa na marafiki wengi ambao amekuwa akipiga nao stori na kumshawishi kwenda kucheza pamoja kama Pacome na Yao.

“Pale Yanga kuna marafiki zangu wengi kuna Pacome, Yao na Aziz Ki hawa wote ni marafiki zangu na tumekuwa tukiwasiliana nao, wamekuwa wakinishawishi kujiunga na Yanga japokuwa tunaongea kwa njia ya utani mara nyingi lakini tukiwa tunapiga stori lazima wataniambia njoo Yanga.

“Tukija kwenye jambo lenyewe la mimi kutakiwa na Yanga ni kweli nimeona tetesi na kwa upande wangu siruhusiwi kuzungumzia jambo kama hilo kwa kuwa kama unavyofahamu mimi ni mchezaji wa Asec kwa sasa na hayo ni mambo ya uongozi wangu na uongozi wa timu, wao ndio wanweza kuzungumzia mambo kama haya,” alisema Sankara

CHANZO CHAMPIONI