ZANZIBAR HEROES V KILIMANJARO STARS KAZINI

KESHO Jumatano, Timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars.

Mchezo huo maalum kwa ajili ya ufunguzi wa Uwanja wa Amaan uliopo Unguja, Zanzibar, baada ya kufanyiwa maboresho makubwa.

Katika kuelekea mchezo huo utakaochezwa saa 2 usiku, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Adel Amrouch, ameita kikosi cha wachezaji 25 ambao jana Jumatatu walitarajia kuingia kambini.

Wakati Kilimanjaro Stars ikiwa na wachezaji 25, Zanzibar Heroes chini ya Kocha Mkuu, Hemed Suleiman Morocco, inajumuisha wachezaji 29, huku juzi Jumapili wakiingia kambini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Kibabu Haji, alisema Kocha Morocco atasaidiwa na Ali Suleiman Mtuli na Mzee Ali Abdallah, huku Saleh Ahmed Machupa akiwa kocha wa makipa.