BENCHIKHA AKUMBUSHWE HAKUNA RAFIKI WA KUDUMU

KWA sasa kwenye vijiwe vya soka iwe mitandaoni mpaka mitaani ni kuhusiana na ujio wa kocha mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha ambaye anatajwa kujiunga na Simba kwa dau kubwa.

Taarifa za awali kupitia vyanzo visivyo rasmi vya Simba vimethibitisha kuwa kocha huyo ameigharimu Simba zaidi ya Shilingi Milioni 500 ili kumwaga wino kwenye timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani.

Sidhani kwa sasa kama kuna shabiki yoyote wa Simba atakuwa anakumbuka mazuri na changamoto za aliyekuwa kocha wao mkuu, Mbrazili Robertinho.

Kocha huyo raia wa Algeria amekuja Simba katika kipindi ambacho timu hiyo ipo kwenye mgawanyiko mkubwa kufuatia mwenendo usioridhisha wa kikosi chao hususani katika michezo yao iliyopita ya mashindano mbalimbali.

Wapo baadhi ya mashabiki wa Simba ambao kutokana na kile kinachoendelea wamefikia hatua ya kugomea kuhudhuria viwanjani kwenye michezo ya timu hiyo wakishinikiza kuondolewa kwa baadhi ya viongozi wa juu wa timu hiyo.

Mkumbusheni, Benchikha kuwa kabla yake alikuwepo Mbrazili, Robertinho ambaye kuna nyakati alipewa ufalme mitaa ya Msimbazi hususani baada ya kuonyesha ubabe wa kupata matokeo mbele ya watani zao wa jadi yaani Yanga.

Mambo yalianza kuwa magumu kwa Robertinho mwanzoni mwa msimu huu na baadaye kuharibika kabisa baada ya kipigo cha aibu cha mabao 5-1 walichokipata kutoka kwa watani zao wa jadi Yanga kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi uliopigwa siku ya Novemba 5, mwaka huu.

Kutokana na kipigo hiko mashabiki wengi wa Simba waliingia hasira na kutaka hatua stahiki zichukuliwe kwa waliosababisha kipigo hicho kuwajibishwa, ndipo viongozi nao wakafanya yao na kumwondoa, Robertinho.

Mkumbusheni, Benchikha kuwa hapa Bongo kuna hali fulani ya unafiki miongoni mwa mashabiki na viongozi wa timu mbalimbali, kwenye nyakati nzuri watakupongeza na kukupa majina yote mazuri, lakini wakikuchoka kibao hugeuka.

Kuna  baadhi ya mifano inaweza kuthibitisha hili kwa kurejea michache unamkumbuka mshambuliaji Mkongomani wa Yanga, Molinga Falcao? Nini kilitokea baadaye? Alikuja Sarpong akawatungua Simba bao kali la mkwaju wa penalti, lakini ilifika kipindi mashabiki wa Yanga ukiwatajia jina la Sarpong wanatamani wakunase makofi.

Kubwa zaidi ni kiungo wa kimataifa wa Ghana, Bernard Morrison ambaye kuna wakati kuondoka kwake Yanga kulitengeneza chuki kubwa kwa mashabiki na alizomewa kila kona na baadaye wakamshangilia baada ya kurudi, halafu wakamzomea tena alivyoachwa.

Njia pekee ya kuzikonga nyoyo za mashabiki wa timu hizi za Simba na Yanga ni kuwapa kile ambacho wanakitaka hususani matokeo kwenye kila mchezo. Timu hizi zina mashabiki wengi ambao wana nguvu kubwa hivyo ukizingua lazima wakumalize.

Narudia tena endeleeni kumkumbusha Benchikha hata Chama na Saido waliimbwa sana viunga vya Msimbazi lakini kwa sasa unasikia wanaitwa ‘Wazee’

Simba wamemisi asali ya mafanikio ambayo wameikosa kwa kipindi cha misimu miwili mfululizo ya utawala wa Yanga kwenye michuano ya ndani.

Kwako Benchikha, Wanasimba wanakupenda lakini kumbuka hawa jamaa hawana rafiki wa kudumu hivyo kesho wakikugeuka ukumbuke na waraka huu kuwa uliwahi kuambiwa.

Wasifu wako ni mkubwa sana nami nina matumaini makubwa kuwa utakuwa na mafanikio makubwa Simba kama ilivyokuwa timu nyingine ulizopita kila la kheri.

Imeandikwa na Mchambuzi wa Kishua, Joel Thomas.