Home Sports WAKIWA ALGERIA, YANGA WASAHAU HABARI ZA USM ALGER

WAKIWA ALGERIA, YANGA WASAHAU HABARI ZA USM ALGER

MOJA ya timu zetu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ipo nchini Algeria kwa ajili ya kuwavaa wababe wan chi hiyo, CR Belouizdad.

Tunakifahamu kiwango cha timu za Algeria na namna ambavyo wamekuwa wakifanya vema huko nyuma.

Hapa katikati timu zao zilionekana kupoteza mwelekeo na kuwaacha Misri na Morocco kutawala kwa muda mrefu.

Kwa sasa, taratibu wanaanza kurejea na mfano mzuri ni USM Alger ambao wamefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho lakini wakawatwanga Al Ahly na kubeba Caf Super Cup.

Mwendo wao unaridhisha kwamba sasa ile nguvu ya Algeria inaanza kurejea na inaonekana hata serikali yao imepania kuona wanasimama na kuwa moja ya mataifa yenye nguvu zaidi kisoka barani Afrika.

Yanga wako ugenini, mara ya mwisho wakiwa Algeria walifanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya wenyeji USM Alger katika fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini mabingwa wakawa wenyeji.

Hii ni sehemu ya hali ya kujiamini kwa Yanga, kwamba wamewahi kushinda ugenini dhidi ya timu ya Algeria, hakuna kinachoweza kuwababaisha.

Ukizingatia mara mbili ndani ya wiki chache zilizopita, USM Alger waliitwanga CR Belouizdad katika mechi ya michuano local.

Hii ni sehemu nyingine ya kuwafanya Yanga waendelee kujiamini zaidi kwamba hakuna kinachoweza kuwashinda licha ya kwamba watakuwa wanacheza ugenini.

Hakika ni jambo zuri kabisa kujiamini unapokuwa ugenini na kuhakikisha unacheza kwa kujiamini na unafanya yale ambayo yanaweza kuonekana ni magumu.

Yanga wanapaswa kujiamini lakini wasijiamini kupita kiasi na inaweza ikawa ni sehemu ya kujenga tatizo kwao.

Nasema hivyo kwa kuwa kwanza lazima tukubali kutofautisha baadhi ya mambo kadhaa. Mfano, CR Belouizdad si USM Alger na kila mmoja ana aina yake ya kupambana katika mechi za kimataifa.

Mechi wanayokwenda kucheza Yanga dhidi ya CR Belouizdad si fainali, mechi ambayo jicho la kila shabiki na hata viongozi liko pale n ahata jukwaa linakuwa limejaa rundo la viongozi wakubwa.

Pia lazima tukubali Ligi ya Mabingwa Afrika haiwezi kuwa kama Kombe la Shirikisho. Kwa hiyo kuna jambo muhimu la kulifanyia kazi hapa.

Litakuwa kosa kubwa sana kama Yanga wataamini inawezekana tu kwa kuwa waliwahi kufanya hivyo yaani kupata ushindi wakiwa katika ardhi ya Algeria.

Bila shaka, CR Belouizdad watakuwa wamechukua tahadhali kubwa sana baada ya kuiona Yanga ikishinda pale Algeria dhidi ya USM Alger.

Achana na hivyo, lazima watakuwa makini sana nah ii itawafanya wajiandae maradufu kuhakikisha wanaivaa Yanga wakiwa imara zaidi.

Bila ya ubishi watu wa Kaskazini mwa Afrika, kwa Afrika Mashariki timu imara zaidi kwao ni Simba ya Tanzania. Lakini wana taarifa ilifungwa mabao 5-1 na Yanga.

Hili hawalichukulii kwa utani tena, lazima itakuwa ni sehemu nyingine ya kujipanga na kufanya maandalizi bora kwa ajili ya mechi inayofuatia.

Kwangu naona Yanga wanakwenda kukutana na mchezo mgumu ambao unawalazimisha kuwa wamejiandaa vizuri.

Litakuwa kosa kubwa sana kama Yanga watauchukulia mchezo huo kama wanauaweza kabla ya kuingia uwanjani.

Litakuwa jambo zuri sana kama tahadhali ya Yanga itakuwa ya kiwango cha juu, halafu wakapambana kama hawajawahi kufika Algeria au hawajui lolote na muhimu wakitaka kushinda.

Inawezekana kabisa, kwa kile walichokipata msimu uliopita licha ya kwamba ilikuwa ni katika Kombe la Shirikisho lakini iwe ni sehemu kubwa sana iliyotumika kuwaimarisha.

Yes, inawezekana lakini haiwezi kuwa nyepesi na lazima kuwe na umakini na mapambano sahihi kuhakikisha wanafanya vema katika mchezo huo kwa kuwa ndio mguu wao wa kwanza katika Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi tokea mwaka 1998.

Previous articleYANGA YAZITAKA POINTI TATU ZA WAARABU KIMATAIFA
Next articleLIGI YA MABINGWA AFRIKA KUANZA LEO KUTIMUA VUMBI,SHINDA MAPENE NA MERIDIANBET