BAADA ya taarifa kueleza kuwa Shirikisho la Soka la kimataifa (FIFA) limeifungia kusajili Klabu ya Simba kutokana na madai ya Klabu ya Teungueth ya Senagal kuhusu malipo ya mchezaji Pape Sakho uongozi wa timu hiyo umekiri kufanya makosa katika kukamilisha mchakato huo.
Ikumbukwe kwamba hivi karibuni rungu la namna hiyo liliwakumba Singida Fountain Gate na mwanzo kabisa wa msimu ni Tabora United walikutana na sakata hilo.
Mapema Novemba 23 Taarifa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ilieleza uamuzi huo uliofanywa na FIFA kuwa ulitokana na Teungueth kushinda kesi ya madai dhidi ya Simba kutokana na mauzo ya Sakho.
Taarifa hiyo ilieleza “Klabu hiyo ilifungua kesi FIFA dhidi ya Simba ikidai sehemu ya malipo kutokana na mauzo ya Sakho. Simba ilitakiwa iwe imetekeleza uamuzi huo ndani ya siku 45 tangu ulipotolewa, lakini haikufanya hivyo,”
TFF imeeleza wakati FIFA ikiifungia Simba kufanya uhamisho wa wachezaji wa kimataifa, wao wameifungia kufanya uhamisho wa ndani.
Uongozi wa Klabu ya Simba uliweka wazi kuwa hakukuwa na mawasiliano na Klabu ya Teungueth ya nchini Senegal iliyoshinda kesi ya madai kuhusu dili la Pape Sakho kwenda Ufaransa.
Taarifa imeeleza: “Malipo ya awamu ya kwanza asilimia 50 yalilipwa Oktoba 2, 2023, klabu ya Simba ilikuwa inasubiri awamu ya pili ili kulipa asilimia 15 ya mauzo kwa klabu ya Teungueth ya Senegal,”
“Klabu ya Simba inakiri kulikuwa hakuna mawasiliano ya Teungueth ya Senegal yaliyopelekea kadhia hii. Hata hivyo Simba inapenda kuujulisha umma kuwa iko mbioni kukamilisha malipo hayo hivi punde,” imeeleza taarifa ya Simba.