UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa malengo makubwa ni kupata ushindi kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya ASEC Mimosas.
Timu hiyo inatarajiwa kusaka ushindi kwenye mchezo huo wa hatua ya makundi Uwanja wa Mkapa Novemba 25 ikiwa ni mchezo wa hatua ya makundi.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa timu zote mbili zinahitaji pointi tatu muhimu.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kazi kubwa itafanyika kwa wachezaji kutafuta ushindi uwanjani.
“Ni mchezo muhimu kwetu kupata ushindi ikiwa ni kampeni za kuelekea kwenye malengo ya kucheza robo fainali kisha tuondoke kwenye hii hatua ambayo tuliishia msimu uliopita.
“Kuna ugumu mkubwa hilo lipo wazi kwa kuwa timu ambazo zimetinga hatua ya makundi zote ni bora. Ili uwe bora ni lazima upate ushindi kwenye timu nyingine ambazo unacheza nazo hivyo tupo tayari na tutapambana kupata ushindi,” amesema Ally.
Novemba 22 Simba imetambulisha uzi mpya kwa ajili ya mashindano hayo ya kimataifa.