MAANDALIZI ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania yakizidi kupamba moto, nyota wa timu hiyo wameahidi wapo kamili kwa mechi zote zilizopo mbele yao.
Simon Msuva anayekipiga Klabu ya JS Kabylie inayoshiriki Ligi Kuu ya Algeria ameweka wazi kuwa wanatambua ugumu uliopo kwenye mechi mbili ambazo ni dakika 180.
Msuva amesema: “Tumekuja kupambania timu yetu ya taifa na tunatambua sio mchezo dhidi ya Niger pekee hapana mechi zote tunazichukulia kwa umuhimu ikiwa ni pamoja na ule dhidi ya Morocco, malengo yetu ni kupata matokeo mazuri. Tunawatambua Niger tuliwahi kucheza nao sio timu nyepesi,”.
Novemba 13 Msuva aliwasili Tanzania akiwa na Haji Mnoga anayekipiga Aldershot Town, Ben Starkie anayekipiga IIkeston Town, Kwesi Kawawa wa Hammarby IF na Msuva walijiunga na kambi kuelekea michezo ya kufuzu Kombe la Dunia.
Itakuwa ni dhidi ya Niger unatarajiwa kuchezwa Novemba 18 ambapo Stars itakuwa ugenini na mchezo wa pili itakuwa dhidi ya Morocco unatarajiwa kuchezwa Novemba 21 Uwanja wa Mkapa.
Ikumbukwe kwamba Novemba 11 wachezaji wa Stars walianza mazoezi rasmi kwa ajili ya mechi hizo muhimu za kuwania Kufuzu Kombe la Dunia.
Miongoni mwa wachezaji ambao walianza mazoezi siku za mwanzo ni pamoja na Feisal Salum, (Fei Toto), Aishi Manula, Beno Kkolanya, Clement Mzize.