BAADA ya kimya cha muda tangu ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 1-5 Yanga, hatimaye ameibuka bosi wa Simba na kuwaomba mashabiki watulie kipindi hiki cha mpito.
Ni Rais wa Heshima wa Simba , Mohamed Dewji amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na minong’ono ya hapa na pale.
Yote hayo ni baada ya kushuhudiwa wakipoteza mchezo wa kwanza ndani ya ligi kwa idadi kubwa ya mabao kutoka kwa watani zao wa jadi Novemba 5, 2023.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Dewji ameandika “Hakika pamoja na uzito, upo wepesi. WanaSimba: Naomba tutulie nakuwa-amini viongozi wetu”
Mbali na kuwaomba utulivu, pia Rais huyo wa Heshima amewaomba mashabiki kuendelea kufika uwanjani kuishabikia timu yao inapocheza.
Kutokana na matokeo hayo Roberto Oliveira aliyekuwa kocha mkuu wa Simba alipewa mkono wa asante na sasa wapo kwenye mchakato wa kumsaka kocha mpya.