SIMBA SC YATAMBA KUWA WA KWANZA KATIKA HILI

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa umefanikiwa kuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kuzindua Simba SC WhatsApp Channel.

Rasmi leo Novemba 14 Simba imetambulisha chanel hiyo ikiwa ni chanzo cha kutoa taarifa kwa mashabiki na dunia nzima kiujumla.

Imani Kujula, Mtendaji Mkuu wa Simba amesema: “Leo tunazindua Simba Sports Club WhatsApp channel. WhatsApp imepakuliwa na watu Bilioni 2.7 duniani ndio mtandao umepakuliwa zaidi duniani. WhatsApp wenyewe walitufata kuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kuwa na chaneli hii.

“Ni timu chache kama Kaizer Chiefs, Al Ahly, Barcelona, Real Madrid na Simba tumejiunga. Katika kuijaribu kabla ya kuzindua ndani ya wiki tumepata wafuasi laki moja. Faida kubwa ni mashabiki kupata taarifa na wadhamini wetu kuonyesha bidhaa zao.

“Hili ni lingine la kwanza kwa Simba kuwa karibu kwa Wenye Nchi. Simba inataka kuja kuwa timu namba moja Afrika na katika hili moja ya sehemu ya kuboresha ni namna ya kutoa habari.

Tunapokuwa na chaneli kama hivi ni sehemu ya Wanasimba na watu wengine kupata taarifa sahihi za klabu. Hii ndio klabu ambayo inafanya vitu vyenye faida na tofauti.

“Ujio wa Simba WhatsApp Channel unakuja na ajira kwa mtu maalumu kuwa na kazi ya kutoa habari.”