KILA timu inaposhuka uwanjani mpango kazi mkubwa ni kupata ushindi. Iwe ni kwenye mchezo wa kirafiki hata ule wa ushindani malengo bado yanabaki palepale kwa kila timu kuhitaji kuwa kwenye mwendo mzuri.
Kwa sasa timu nyingi zipo kwenye maandalizi kwa ajili ya mechi za kitaifa na kimataifa hilo lipo wazi. Zipo ambazo malengo makubwa ni kwenye mechi za ligi na nyingine ni kwenye upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kila idara inatambua majukumu yake ya kufanya na mashindano yote yanamipango tofauti. Mbinu za kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni tofauti na ile ya kwenye ligi.
Ambacho kinahitajika kwa sasa kwenye kila idara ni kupambana na kupata matokeo mazuri bila kujali mchezo wao watacheza wakiwa nyumbani ama ugenini.
Kushinda ugenini na nyumbani kunaongeza nguvu ya kusonga mbele kwenye hatua ambayo timu husika ipo. Ukitazama wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa kazi yao ni kuondoka katika hatua ya makundi.
Mpango kazi makini unahitajika kwa Simba na Yanga kujiondoa kwenye hatua hiyo waliyopo kwa kufanya kweli na kupata matokeo kwenye mechi zao zote watakazocheza.
Kazi kubwa kwenye hatua ya makundi ni kusaka pointi tatu muhimu. Hizi ni muhimu kwatimu kuwa makini kuzitafuta ili kufikia malengo ya kutinga hatua ya robo fainali.
Isiishie hapo tu ni muhimu kuwa na mwendelezo bora bila kuhofia mnacheza mkiwa nyumbani ama ugenini muhimu kupata matokeo chanya na inawezekana kwa kuwa mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi na mbinu.