Home Sports HUU WAKATI SAHIHI MASHABIKI SIMBA WAAMUE KUWA DAWA AU SUMU

HUU WAKATI SAHIHI MASHABIKI SIMBA WAAMUE KUWA DAWA AU SUMU

HAKUNA ubishi, huu ndio wakati mashabiki wa Simba wanapaswa kuonyesha ukomavu wao baada ya mambo kwenda mlama.

Kipigo cha bao 5-1 ambacho walikipata kutoka kwa watani wao wa jadi Yanga, hakikuwa cha kutarajiwa.

Hakuna shabiki wa Yanga alitarajia timu yake ingekuwa na uwezo wa kushinda kwa mabao Matano dhidi ya Simba.

Kwa upande wa Simba pia, hakuna shabiki angeweza kukubali kama ungemwambia timu yake inaweza kupoteza kwa idadi ya mabao Matano dhidi ya watani wao Yanga.

Lilikuwa ni kama pigo la kushtukiza kwa kuwa mashabiki wa Simba, sasa ni miaka 12 wamekuwa wakijitapa na ushindi wao wa mabao 5-0 waliowachapa Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa.

Sasa, kisasi kimelipwa. Tena imetokea katika kipindi ambacho suala la kuwaza kuwa kesho au leo kisasi kitalipwa, hakuna aliyekuwa akifikiria.

Baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, Kocha wa Simba wakati huo, Milovan Cirkovic aliniambia; “Matokeo kama haya ni vigumu sana kutokea kwa hivi karibuni, angalau miaka 10 ijayo kinaweza kutokea kitu kama hiki.

“Mara nyingi matokeo haya hutokea kama ilivyo leo, hakuna aliyetarajia. Hata mimi nilitaka kushinda dhidi ya Yanga lakini sikuwa na hesabu ya ushindi wa mabao haya Matano, maana kikosi chao ni bora, huwezi kupiga hesabu ya kuwafunga idadi hiyo ya mabao ikawa kwenye mpango wako.”

Hata ukimuuliza Kocha Gamondi wa Yanga, hawezi kukuambia alikuwa kwenye mpango huo wa kushinda mabao Matano dhidi ya Simba, hii ndio soka.

Sasa kwa mashabiki wa Simba, haliwezi tena kuwa jambo ambalo litafutika baada ya mechi 10 zijazo au mwaka mmoja au miwili. Ni jambo ambalo lazima wakubali kuishi nalo kwa sasa na ndio kipindi ambacho wapaswa kuonyesha ukomavu wao.

Wana haki ya kusema ukweli, kama wanalalamika, kama wana maoni, huu ndio wakati wao na wanapaswa kusema kweli.

Bila ya ubishi lazima wana uchungu, maana kupoteza ni jambo la kawaida lakini kila unayemsikia anazungumzia idadi ya mabao.

Yes, lakini wakati wakiendelea kulalamika na kutoa machungu yao, lazima wawe na njia sahihi ambayo wanapitia kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri katika klabu yao baada ya kuteleza.

Mechi muhimu kwa Simba haikuwa hiyo moja, kuna mechi nyingine za ligi na kama wakifanya mchezo, kuanzia mechi ya jana dhidi ya Namungo itakuwa ngumu sana, baada ya hapo zifuatazo pia zitakuwa mtihani mgumu kwao.

Wakati wamekosea, lazima wajue wakati mwafaka wa kutoa machungu yao bila ya kuvuruga safari inayoendelea.

Kama umepoteza dhidi ya Yanga, unakubali kuwa chanzo cha kuifanya timu yako isitulie na kupoteza au kutofanya vizuri kwenye mechi nyingine za ligi au Ligi ya Mabingwa Afrika?

Simba imeteleza na kuwaumiza mashabiki wake, huenda sasa maumivu hayo yanaweza kuwa chachu ya marekebisho makubwa kuanzia kwa uongozi, benchi la ufundi lakini wachezaji wenyewe.

Sasa mashabiki ambao wameumiwa wanaweza kuwa DAWA au SUMU? Hili ni chaguo la mashabiki wenyewe kwamba wanataka kuwa akina nani katika klabu yao katika kipindi hiki.

Mashabiki wakiamua kuwa dawa, watatibu hali iliyopo, marekebisho yatafanyika na Simba itarejea ten ana kupambana kuwania ubingwa.

Kama mashabiki wataamua kuwa sumu, pia inawezekana n ani uamuzi wao lakini ndio kitakuwa chanzo cha Simba kuendelea kuboronga na kufanya vibaya zaidi na hii itaendelea kutonesha jeraha la kipigo cha tano kutoka kwa watani wao.

Previous articleMSHINDI WA MILIONI MOJA KUTOKA VIBUNDA SPESHO PARIMATCH NA TIGO PESA LEO
Next articleMUUNGANIKO WA KAZI YANGA WAPEWA ZIGO JINGINE