Home Sports KUPIGANA UWANJANI NI USHAMBA, MUDA WAKE UMEISHA

KUPIGANA UWANJANI NI USHAMBA, MUDA WAKE UMEISHA

JUMA lililopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Ihefu FC kuna kipande cha video kilisambaa kikionyesha kundi la mashabiki wa Simba wakimshushia kichapo shabiki aliyefahamika kuwa ni wa Yanga kutokana na rangi ya mavazi yake.

Vitendo hivi kuna nyakati vilishamiri na tulipaza sauti vikapotea lakini hivi sasa vinaonekana kurejea tena kwa kasi kubwa. Ligi Kuu Bara ni miongoni mwa ligi ambazo zinatazamwa kwa ukubwa hivi sasa karibu kila kona ya bara letu.

Wapo watu wanasafiri maili nyingi kuja kushuhudia mechi zetu hivyo kuanza kwa vitendo hivi visivyo vya kiungwana michezoni kwa kiasi kikubwa vinatuwekea dosari kwenye mpira wetu na tunapaswa kulikemea hili kwa nguvu kubwa.

Mchezo wa soka ni mchezo wa hisia hivyo wewe kama shabiki unapaswa kujua ukomo wa mihemko yako ili kutosababisha matatizo kwa wengine mnapaswa kujua kwenye mchezo wa soka kuna pande mbili.

Upande wa kwanza ni ule unaozomea na upande wa pili ni ule unaoshangilia hivyo kama upo kwenye upande wa kuzomea zomea lakini kwa kuzingatia miiko na kama upo kwenye upande wa kushangilia pia shangilia kwa kufuata miiko.

Ukiachana na tofauti zetu kiitikadi kwa maana huyu Simba, yule Yanga na mwingine Prisons asilimia kubwa sisi wote tunaishi eneo moja ama maeneo jirani si ajabu kukuta nyumbani baba ni shabiiki wa Yanga mama shabiki wa Simba na watoto wanashabikia aidha Simba au Yanga.

Hivyo baada ya soka lazima maisha mengine yaendelee hivyo si jambo jema kuona mpira ambao ni mchezo unaotuunganisha na kutuleta pamoja unageuka chanzo cha vita baina yetu.

Sisi ni ndugu, sisi ni familia moja hivyo ni lazima tulindane wenyewe kwa wenyewe pia tuwe mabalozi wa kuhubiri amani kupitia michezo, ni wazi huenda kuna watu wanatamani kuwa sehemu ya maelfu yanayojitokeza viwanjani kutazama mechi hizi hivyo tukianza kuwaonyesha matendo haya ambayo ni kinyume na uanamichezo bila shaka yoyote tutakwenda kuwapoteza wote.

Wikiendi hii kuna mechi kubwa ya Watani hii ikawe sehemu ya sisi kutangaza amani kwa vitendo. Ni mechi ambayo inakutanisha mashabiki kutoka kila kona ya nchi na nje ya nchi hivyo hatutarajii kuona taswira nzima ya mchezo inakwenda kuharibiwa na kundi la watu wachache wenye nia ovu ya kuupaka tope mpira wetu.

Rai yangu kwa wasemaji na maofisa habari huenda wachambuzi wenzangu hawajawaambia lakini nyie ni miongoni mwa watu ambao kwa kiasi kikubwa mnachangia matukio ya aina hii kutokea viwanjani kutokana na kauli zenu ambazo mnapaswa kuzichuja kabla ya kutoka mbele ya vipaza na kuongea.

Mnapaswa kutambua mnaongoza maelfu ya wanachama na mashabiki ambao kila mmoja ana namna yake ya kupokea ujumbe anaoletewa.

Chungeni kauli zenu hizi pia zinachangia na kuhimiza chuki miongoni mwa mashabiki wenu nyie ndio mnapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha amani inatawala kwenye michezo yenu na si kuwa visababishi vya chuki kwa mashabiki wenu.

Tuachane na tabia hizi za kishamba za kupigana viwanjani zilishapitwa na wakati uhuni wa aina hiyo hauna nafasi tena kwenye soka la sasa.

Previous articleKI KAWAPOTEZA WENGINE NDANI YA YANGA
Next articleKOCHA YANGA AWASOMEA RAMANI SIMBA DAKIKA 180