UKIWA KWA MKAPA ONYESHA UKOMAVU, AL AHLY HAWAJAWAHI KUWA WEPESI

HATIMAYE siku imewadia, ni leo pale kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, historia inakwenda kuandikwa.

Simba, itaandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza michuano mikubwa na mipya ya African Football League ikiwa na Al Ahly ya Misri.

Kwa mechi lazima tukumbushane, kwamba hata kidogo haitakuwa nyepesi kama ambavyo watu wamekuwa wakiielezea kwa marejeo ya mechi zilizopita.

Kweli, Simba wamekuwa wababe wa Ahly kila mara wanapocheza katika ardhi ya Tanzania lakini lazima kujikumbusha pia kuwa hadi Simba walifanikiwa kufanya vizuri katika mechi hizo hapa nyumbani, walijipanga hasa.

Kujipanga hasa ni pamoja na kuwa na maandalizi sahihi na kikosi kikaifanya kazi yake vizuri sana uwanjani.

Ahly haijawahi kuwa timu nyepesi na hasa inapocheza katika nchi yoyote barani Afrika, wao ndio wanakuwa ni wababe kwa kuwa ndio klabu namna moja na kubwa barani Afrika.

Pamoja na hivyo, wanautambua ubora wa Simba na watajipanga na wanatambua wanatakiwa kuandika rekodi mpya kwa kuwa mashindano ya African Football League ni mapya na makubwa na rekodi zinatakiwa kutunzwa.

Maana yake watataka kuanza vizuri katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo ambayo ni bahati kubwa imepangwa ianze na kufunguliwa katika ardhi ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.

Wakati Simba wanapambana uwanjani, niwakumbushe kuwa kwa yeyote atakayefanikiwa kuingia uwanjani, ana jukumu la kuiheshimisha Simba na Tanzania.

Ataiheshimisha vipi, mchezo lazima utakuwa mgumu. Matarajio ya Wanasimba kwa kikosi chao ni makubwa sana, hivyo tofauti na hapo wako wanaweza kushindwa kuwa na utulivu.

Hakikisha unakwenda uwanjani bila ya kuwa na matokeo ya mfukoni, kuamini unakwenda UWanja wa Mkapa kuiangalia Simba ikishinda ni makosa makubwa na si sifa za shabiki wa soka.

Yes, Simba wako nyumbani, kweli mechi nyingi dhidi ya Ahly nchini wameshinda lakini hii si gerentii kuwa ni lazima watashinda na leo. Bila shaka Simba wana timu nzuri na ina uwezo wa kutoa upinzani wa juu kabisa kwa vigogo hao wa Afrika.

Pamoja na hivyo, matokeo yanaweza kuwa mazuri yakafurahisha kila aliyekwenda uwanjani na aliyeamini au kutamani kuiona Simba ikishinda mchezo wake huo wa kwanza wa African Football League.

Pia inaweza kuwa tofauti kwa juwa hii ni football, mambo yanaweza kuwa tofauti kabisa na matarajio ya wengi na Simba akapoteza au kutoka sare.

Unapokwenda uwanjani, kuwa tayari na matokeo. Inawezekana ikawa ushinda, sare au hata kupoteza. Na ikiwa ni upande wa furaha, basi sherekea kistaarabu na hakikisha unatoka hapo kurejea nyumbani ikiwa ni sehemu ya waliodumisha amani na upendo.

Ikiwa imetokea umepoteza, amini ndio mpira na baada ya mechi, toka uwanjani kwa kufuata utaratibu na urejee nyumbani kwa amani na upendo.

Hata baada ya mechi hiyo, bado heshima ya Tanzania inapaswa kuwa juu, heshima ya Simba inapaswa kuapanda pia.

Heshima ya Simba haipandishwi na ushindi na mafanikio pekee, mashabiki wake ni sehemu ya heshima hiyo na lazima waonyeshe ni mashabiki wa mpira hasa wanaojitambua na kuutambua mpira.

Haipaswi kufanya matukio ambayo yanaonyesha kuna watu wa hovyo, wenye jazba,m wasiosikiliza.

Caf wanaamini sana sehemu yenye muonekano wa soka, sehemu yenye usalama na uhakika kwa mashabiki wanaojumuika uwanjani. Wameichagua Tanzania kwa kuwa wanajua pamoja na kuwa na Simba lakini wana nafasi kuungana na mashabiki wastaarabu, waelewa wa soka wa klabu hiyo.

Acha wageni waondoke na kama tutakuwa na mambo yetu yenye maudhi, basi tutaendelee na maisha yetu.

Vizuri kushangilia kwa nguvu na kuiunga mkono Simba, vizuri kushangilia bila ya kumuumiza au kumdhuru mwingine yeyote na hili linawezekana kwa kuwa kadhaa yaliyowahi kutokea yanaweza kuwa sehemu ya mafunzo na kuwafanya mashabiki wa soka nchini, kuwa imara zaidi bila ya uhatarishi wowote.