Home Sports SIMBA V AL AHLY, HISTORIA NYINGINE INAKWENDA KUANDIKWA

SIMBA V AL AHLY, HISTORIA NYINGINE INAKWENDA KUANDIKWA

HISTORIA inakwenda kuandikwa kwa Simba kuwa wafunguzi wa African Football League ambapo leo Oktoba 20, 2023 mchezo wa ufunguzi unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.

Chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira Simba itakuwa na kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly kutoka Misri ambao nao pia wanahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa mipango inakwenda vizuri na wanahitaji kuonyesha ukubwa wao kwenye mchezo huo mkubwa:-

“Tunakwenda kuonyesha ukubwa wetu kwa kucheza na timu kubwa Afrika na yenye rekodi bora hilo lipo wazi. Simba inaingia kwenye orodha ya timu bora na zenye rekodi kubwa pia itakuwa hivyo.

Kipi kinawapa nguvu ya kupata ushindi?

“Ubora wa wachezaji tulionao unatupa nguvu ya kuamini kwamba tutaleta ushindani na kupata matokeo kwenye mchezo ndani ya dakika 90.

“Unapozungumzia Al Ahly sio timu ndogo hilo lipo wazi na tunalitambua. Tuna wachezaji wanatambua ugumu wa mashindano ya kimataifa na wana uzoefu.

“Yupo Fabrince Ngoma yeye ni kiungo mwenye uwezo mkubwa kwenye kutoa pasi elekezi. Luis Miquissone anawatambua na aliwahi kuwafunga Uwanja wa Mkapa. John Bocco, Clatous Chama hawa ni baadhi ya wachezaji wetu ambao wanashauku kuona tunapata ushindi.

Hali za wachezaji zipoje?

“Kiujumla wachezaji wanazidi kuimarika, unaona kipa wetu Aishi Manula aliyekuwa nje kwa muda karejea akianza mazoezi na wenzake hii inamaanisha kwamba tunazidi kuwa imara kwenye upande wa eneo la ulinzi.

“Kurejea kwa Manula kunampa machaguo kocha wetu Roberto Oliveira kujua nani ataanza kikosi cha kwanza kulingana na mechi husika na wengine waliopo hali zao zipo vizuri.

Kucheza na timu kubwa ugumu upo wapi?

“Ugumu upo kwa kuwa hata wao wanapata ugumu kupambana na wakubwa wenzao kwenye haya mashindano. Tupo nyumbani kwenye uwanja ambao tumetoa hela pia kwenye marekebisho yake hapo unadhani itakuwa kazi kubwa kwetu?

“Ili uwe mkubwa lazima upate ushindi mbele ya mkubwa nasi tunataka nafasi ya Al Ahly ya ubora barani Afrika kuwa namba moja tunaamini tunaweza kuifikia. Hakuna kinachoshindikana tukiwa tunahitaji jambo letu.

“Kwenye ubora wake Al Ahly tulishamfunga kwenye mashindano ambayo tulikutana nayo na kwa wakati huu wamekuja wakati mbaya ambao tunataka sifa Afrika, hakika hatutamuacha salama.

Ushiriki wenu ulitokana na nini?

“Ukubwa wetu, haikuwa kazi ndogo, tumefanya kazi kubwa sana kuipata nafasi hii. Mtu wa kawaida anaweza kufikiria kwamba CAF walitaka kila timu kutoka kila nchi ukweli wao walitaka timu bora kutoka kila ukanda.

“Yaani CAF wakianzisha mashindano ya timu nne sisi tutakuwepo. Wengine kupata nafasi lazima mashindano yawe na timu 20 kwenda mbele. Watakuja wageni wengi ikiwa ni pamoja na Ifantino, (Gianni Rais wa FIFA)  pamoja na viongozi wengine kwa hili tuna haki ya kujidai kwa kweli.

“Wakati ujao tunaamini timu zitaongezeka na wengine watashiriki mpaka Ihefu wanaweza kupata nafasi ya kuwa kwenye mashindano haya makubwa ila kwa sasa sisi tunaanza kuandika rekodi hii na tumepata hesima mashindano yanafunguliwa Uwanja wa Mkapa, nyumbani.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani za kutosha kwa kuwa kutakuwa na mambo mengi mazuri kwa ajili yao mbali na kushuhudia mchezo mzuri kutoka kwa wachezaji wetu,” amesema Ally.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, (Dizo Click) na kutoka gazeti la Spoti Xtra Alhamisi

 

Previous articleYANGA V AZAM KITAUMANA KWA MKAPA
Next articleUKIWA KWA MKAPA ONYESHA UKOMAVU, AL AHLY HAWAJAWAHI KUWA WEPESI