SIMBA IMETUBEBA TUIPONGEZE NA SI KUIBEZA, LAKINI UKWELI USEMWA

TANZANIA ina sababu nyingi sana kujivunia kurejea kwa Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nafasi ambayo waliikosa kwa kipindi cha miaka 25, umri wa kijana mwenye familia. Halikuwa jambo dogo na sasa wamerejea tena.

Simba, imekuwa timu pekee ya Tanzania ambayo imekuwa ikifanya vizuri mfululizo na tegemeo kwa timu za Tanzania na Afrika Mashariki.

Heshima ya Afrika Mashariki ilibebwa na Simba, ilikuwa timu pekee inapambana na timu kutoka Kusini, Magharibi na Kaskazini.

Hii ilikuwa ni baada ya timu za Sudan kwa maana ya Al Hilal na Merreikh kuanza kupoteza nguvu yao iliyozoeleka.

Sasa mambo yamekwenda tofauti, kwa kuwa Yanga nao wameamka na tumeona kuanzia msimu uliopita walikuwa katika hatua ya makundi, wakaingia mtoano hadi kwenda fainali.

Hawakufanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho, hata hivyo heshima yao walitakiwa kupewa kwa kuwa kufikia hatua hiyo, mara ya mwisho kwa timu za Tanzania ilikuwa ni mwaka 1993 wakati Simba ilipocheza fainali ya Kombe la Caf na kupoteza dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Sasa Tanzania ina Simba na Yanga, timu mbili kwa wakati mmoja kwenye hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, haijawahi kutokea.

Yanga walionyesha mapema wanaitaka hii nafasi, wamefanikisha. Simba walikuwa wanaendelea kuonyesha wana uhakika wa kusonga mbele kama kawaida yao na wamefanya hivyo.

Hata hivyo kumekuwa na mjadala kuwa Simba wamevuka kwa ugumu, wengi wameshangazwa lakini lazima kukubali mambo kadhaa na kuanza kuwapa Simba heshima yao.

Wamevuka dhidi ya bingwa wa Zambia, Power Dynamo ambao wamewahi kuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho, si timu ndogo.

Ukweli tuwaambie, kuwa uchezaji wao hasa katika dakika 45 za mchezo, wachezaji hawakuonyesha walikuwa wameutaka mchezo na wanakwenda kufuzu. Hawakuonyesha wako tayari na wana njaa. Lakini kweli wamefuzu.

Kuwaeleza ukweli kuwa wanatakiwa kujituma na kuonyesha ni askari wanaotaka kushinda wakiwa na jezi ya Simba, ni jambo zuri sana kwa kuwa mashabiki hufika uwanjani kuonyesha wamekwenda kuwaunga mkono na wanautaka ushindi.

Lazima kusema ukweli, lazima kusisitiza kweli kulikuwa na walakini na wachezaji kuna jambo wanapaswa kubadilika na Kocha Robertinho kuna mambo anatakiwa kuyafanyia kazi kwa kuwa wanakwenda kwenye hatua ngumu zaidi.

Msimu uliopita walitoka hatua ya makundi kwa kupoteza mechi mbili za mwanzo na baada ya hapo wakajitutumua na kwenda kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya robo fainali na wakaishia hapo.

Simba wamefuzu tena, wamefanya Tanzania iwe na timu mbili kama ilivyo kwa Misri waliozivusha Al Ahly na Pyramids na Tunisia wenye Esperance na Etoile du Sahel. Hakuna timu nyingine ya Afrika imeingiza timu mbili.

Jumla ya timu zilizovuka ni 16, Tanzania, Misri na Tunisia zimechangia timu sita na zilizobaki ikiwemo Morocco ni timu moja tu. Kumbuka hata mabingwa wao FAR Rabat wametolewa na Sahel ya Tunisia.

Ndio maana nikawa nasisitiza, kuwa tuwaambie Simba ukweli bila ya woga hata kidogo lakini wakati tukisema hayo lazima tukumbuke kuwapa heshima yao kuwa kuna jambo wamefanya.

Lengo la kuingia hatua ya makundi limefanikiwa na kwao safari waliyoitangaza hawajaifikia maana walisema mapema tu kuwa wanataka kwenda hadi nusu fainali. Yanga wakasema nia ni kuingia makundi na wamefanikiwa, huenda nao wakatangaza safari mpya kwenda robo fainali au zaidi.

Hivyo kuna jambo ambalo wamelifanya Simba na Yanga safari linapawa kuchukuliwa chanya na si vinginevyo. Lakini kwa kuwa tunatambua hatua zinazofuata ni ngumu zaidi, kuwakumbusha si vibaya, kuwaeleza ukweli si vibaya lakini si sahihi kuwaonyesha kuwa kama wameshafeli kabisa.