KIMATAIFA FANYENI KWELI KAZI BADO IPO

KUPEWA majukumu katika timu Bongo kwa wachezaji ni jambo muhimu kuzingatia na kila mmoja kufanya kwa wakati kile kinachotakiwa ndani ya uwanja.

Kwenye mechi za kimataifa hapo nguvu kubwa zinahitajika mbali na uwekezaji na wachezaji nao wanapaswa kujituma bila kuogopa.

Tumeshuhudia namna Singida Fountain Gate walivyopenya hatua inayofuata kwenye Kombe la Shirikisho kwa kupata upinzani kutoka kwa JKU.

Hapa Singida Fountain Gate wanatoa somo kwama mchezo wa kumaliza kazi ni ule wakwanza kisha wa pili hautabiriki kutokana na matokeo yatakavyokuwa.

Benchi la ufundi litakuwa limeona makosa yalipo ndani ya Singida Fountain Gate hivyo wana kazi ya kuboresha pale ambapo walifanya tofauti.

Yanga wao wamesonga mbele kwa ushindi wa mabao 7-1 ASAS FC bado kazi haijaisha kwa kuwa ni muhimu kufanya maandalizi kwa mechi zijazo ili kuendelea kuwa katika ubora.

Ngumu kuamini kwamba kwenye mechi za nyumbani na utajiri wa mashabiki kazi kubwa inakuwepo tena katika kutafuta matokeo.

Muhimu kwa timu nyingine ambazo zimebaki kwenye mashindano ya kimataifa kufanya maandalizi mazuri kwenye kila idara.

Tunaona kete ya kwanza Azam FC imeshagota mwisho kutoka kwenye Ligi Kuu Bara zikiwa zimebaki timu tatu ambazo ni Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Singida Fountain Gate katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Muda uliopo kwa sasa kwa Azam FC sio wa kumtafuta mchawi nani bali kuongeza nguvu kufanyia kazi makosa yaliyotokea kuanzia mechi ya kwanza na ya pili.

Wachezaji na benchi la ufundi ni muhimu kutambua kwamba kinachotafutwa kwenye mechi hizi za kimataifa ni ushindi ikiwa ushindi umepatikana kuna ulazima wa kuongeza nguvu kwenye ulinzi.

Kutolewa kwa changamoto za penalti ni maumivu kwa mashabiki na viongozi huku wachezaji wao wakikwama kutimiza malengo ya timu pamoja na malengo ya mchezaji mmojammoja hivyo ni muda wa kuangalia wapi walikosea kwa mara nyingine.

Timu ambazo zimebaki katika anga la kimataifa ni muhimu kufanya kazi kwa umakini kuwapa furaha mashabiki na kutimiza majukumu kwa umakini.