CHUMA KIPYA SIMBA KINA BALAA HICHO

CHUMA kipya ndani ya kikosi cha Simba ni kiraka kutokana na kupanda na kushuka kwenye kutimiza majukumu yake ndani ya uwanja.

Nyota huyo anatambua kwamba msimu wa 2022/23 ni Yanga walitwaa taji la Ligi Kuu Bara huku Simba wakigotea nafasi ya pili.

Ikumbukwe kwamba Julai 9, Che Malone Fondoh ambaye ni beki raia wa Cameroon akitokea Cotton Sports alitambulishwa Simba kuwa ingizo jipya.

Beki huyo moja kwa moja ameingia kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mkuu Roberto Oliveira aliyemtumia kwenye mechi zote mbili za ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji.

Pia alikuwa miongoni mwa wale ambao walicheza fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga pale Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Che Malone mbali na makosa anayofanya katika mechi za ligi ikiwa ni pamoja na kushindwa kuulinda mpira dakika ya 19 dhidi ya Mtibwa Sugar ulioleta bao lililofungwa na Matheo Anthony dakika ya 20 alikuwa akiwazuia wapinzani wake.

Mbali na kuwazuia wapinzani hao kwa kukaba chuma hicho kipya kilikuwa kinapanda mbele kupeleka mashambulizi kama alivyofanya kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.

Kwenye mechi mbili za ligi ni shuhuda mabao mawili yakizama kimiani ambapo ni kipa Ally Salim alikuwa langoni.

Anafanya kazi kwa ushirikiano na Kennedy Juma huku Henock Inonga akipambania hali yake kwa kuwa alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate.