Home Sports HAKI MUHIMU KUZINGATIWA NDANI YA LIGI KUU BARA

HAKI MUHIMU KUZINGATIWA NDANI YA LIGI KUU BARA

KASI ya Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa kwanza imekuwa kubwa na kila timu inaonyesha ushindani wake ndani ya dakika 90 kusaka ushindi hili ni jambo kubwa na muhimu.

Sio Singida Fountain Gate, Namungo wala Ihefu zote zinapambana kufanya kweli hata zile ambazo zimepanda msimu huu kutoka Championship ikiwa ni Mashujaa na JKT Tanzania.

Kila timu ina nafasi ya kupata matokeo na tumeona kwenye mechi za nyumbani ama ugenini timu zinashinda na zote ni zile ambazo zinatumia nafasi kwa umakini

Ni ligi bora ambayo kila mchezaji anapenda kuonyesha  ubora wake uwanjani inapaswa kuwa hivyo mpaka mzunguko wa pili kwa wachezaji kuendeleza ubora wao.

Iwe hivyo kwenye mechi zote ambazo zinachezwa kwani ligi ya Tanzania ni miongoni mwa zile ambazo zinafuatiliwa kwa ukaribu kutokana na kukua kwake.

Hakuna ambaye anapenda kuona timu yake inashindwa kupata matokeo uwanjani lipo wazi hivyo kurejea kwa ligi iwe ni mwendelezo wa yale mazuri ambayo wengi wanatarajia.

Isije ikawa ligi inarudi kisha wachezaji wengi wakaanza kupelekwa kupewa matibabu kwa sababu wameumizwa na wachezaji wenzao uwanjani.

Hili sio sawa mpira una migongano hilo lipo wazi lakini sio kila mchezaji lazima atembeza mikato ya kimyakimya kwa mchezaji mwenzake hata pale isipotakiwa.

Nidhamu kwenye kila mchezo ni muhimu na hii itawafanya wachezaji kupata matokeo mazuri na timu kupata ushindi bila kuwa na makelele.

Kwa upande wa waamuzi kazi ni moja kusimamia haki kwenye kila mchezo. Herufi zake ni chache ukizitazama neno haki lakini utekelezaji wake unakuwa na ugumu kwenye maamuzi.

Msimu mpya uwe na utofauti kwenye kila jambo kuanzia wachezaji mpaka waamuzi bila kusahau mashabiki ni muhimu kufuata haki.

Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpangilio mzuri na maamuzi kuwa ya haki kwenye mechi zote ambazo zinachezwa.

Ikiwa makelele yataanza mapema hii sio sawa kwa kuwa mpira ni burudani iwe ni kwa wale wanaoshinda hata wanaoshindwa nao wanapenda kuona burudani.

Mashabiki suala la kugombana nje ya uwanja muda wake umegota mwisho amani itawale kila kona.

Ukipoteza ni muda wa kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao na ukishinda pia haina maana kwamba mipango itakuwa imekwisha kazi inapaswa kuendelea.

Previous articleKAGERA SUGAR YAANZA KWA MWENDO WA KUSUASUA
Next articleVIDEO: JEMBE AFUNGUKIA KIPIMO CHA AZAM FC/ YANGA V SIMBA