LIGI IMEANZA NA UKIMYA, WAAMUZI MSINYONGE HADHARANI TENA

  TUPO kwenye Ligi Kuu Bara, kipindi ambacho kilikuwa kinasubiriwa kwa hamu kubwa ikiwa ni msimu wa 2023/24.

  Mashabiki wa mpira nchini walisubiri kwa hamu kubwa kuona ligi inaanza tena. Hilo likatokea na tumefanikiwa kuona mambo yakienda vizuri sana.

  Ligi imekuwa na msisimko mkubwa licha ya kwamba, mabingwa watetezi Yanga wameshindwa kuanza mechi za ligi baada ya kupewa nafasi ya kujiandaa katika michuano ya kimataifa.

  Mechi yao ya jana ikiwa ni hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ndio walikuwa wanaanza kazi dhidi ya Telecomunication ya Djibouti.

  Wawakilishi wengi wa Tanzania katika michuano hiyo, Simba wao wataanzia hatua inayofuata, hii ni kutokana na pointi walizozikusanya na zinawafanya wawe na nafasi hiyo pamoja na timu nyingine kubwa za Afrika.

  Wakati Yanga hawajaanza ligi katika mechi ya pili sasa, wengine wameanza na unaona. Kama kutakuwa na mapungufu basi yatakuwa machache ya kibinadamu.

  Hapa sigusi yale mapungufu ya uzembe yaliyofanywa na uongozi wa klabu ya Kitayose kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji wake.

  Nazungumzia mengi, kwa maana ya viwanjani na kadhalika. Lakini zaidi leo kwa mara nyingine bila kuchoka nagusia suala la waamuzi.

  Hakuna matukio ya kukera kwa uzembe, matukio ambayo kama unayakumbuka yalikuwa rundo katika mzunguko wa kwanza wa msimu uliopita.

  Malalamiko ya timu nyingi sana yalikuwa makubwa. Waamuzi walifanya makosa makubwa mengi yaliyopitiliza.

  Hakika yalikuwa makosa yanayojirudia kwa baadhi ya timu dhidi ya timu ambazo zilipolalamika hakukuwa na ubishi ulikuwa ukweli mtupu.

  Faida ya mikwaju ya penalti ambayo wazi ilionekana ilikuwa kuna walakini mkubwa na wa wazi. Kuna timu zilifaidika na kukawa na marudio ya timu hizo kufaidika na kupatikana kwa mikwaju hiyo lakini ya uonevu.

  Kuna viwanja vilikuwa maarufu, wanapocheza wenyeji, waamuzi “walinyonga” hadharani bila ya woga. Jambo ambalo halikuwa sahihi hata kidogo na bado wakaendelea kufanya hivyo.

  Hakuna tunachoweza kukataa kwamba rushwa ipo, tunajua tayari Takukuru wamesema wameingia na watashirikiana na TFF katika hili lakini lazima tuwe wakweli, kazi ni ngumu kwa kuwa wanaotoa na wanaopokea “wote wanafurahia”.

  Hivyo inakuwa kazi ngumu kwao kuzuia hili au kuwapata hawa watu ambao wamekuwa na tabia hizi mbovu na si za kuiungwana ambazo zinaharibu mpira wetu.

  Nimeona leo itakuwa ni nafasi nzuri ya kuwakumbusha, kwamba baadhi ya waamuzi waliposimamishwa, mambo yakatulia na tukaenda kwa mwendo mzuri sana.

  Haikuelezwa lakini ukweli wako walikuwa kama mawakala wa baadhi ya klabu ambazo zilifaidika sana na “wizi wa hadharani”.

  Inawezekana wamerejea na inawezekana wakawa wameahidi kwamba wamejirekebisha kwa nia ya kuhakikisha wanafanya vema baada ya kuweka sawa mienendo yao mibovu.

  Sijajua kama TFF na Kamati ya Waamuzi watakuwa wamewarudisha. Na kama itakuwa ni hivyo basi tuwaonye mapema kwa kuwa bado tuna kumbukumbu mbovu dhidi yao.

  Tunawakumbusha waache kufanya makosa ya makusudi na kuyaita makosa ya kibinadamu. Tunawakumbusha kuacha kuuharibu mpira wa Tanzania kwa makusudi kwa maslahi yao binafasi.

  Mwisho, mimi niwakumbushe kuisimamia haki kwa dhati kama ambavyo walivyoaminiwa kuwa watafsiri wa sheria 17 za mchezo wa soka uwanjani.

  Jukumu ni kubwa na haki inatakiwa kupita kiasi. TFF hawatachafuka kama waamuzi watakuwa bora na wakumbuke, ligi yetu sasa ni maarufu zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hivyo haipendezi kuwa na gumzo la maamuzi mabovu kutoka kwa waamuzi walioaminiwa na kamati ya waamuzi na wakapewa kazi chini ya shirikisho la soka.

  Ninaamini kuna nafasi kubwa mambo yakawa sahihi na bora kama waamuzi wataifanya kazi yao kwa weledi. Niwakumbushe, mpira unachezwa hadharani na makosa yote yanaonekana wazi kuwa ni ya kibinadamu au makusudi kwa maslahi binafsi.

  Ameandika Saleh Ally Jembe

  Previous articleBEACH SOCCER NI MWENDO WA VICHAPO TU
  Next articleVIDEO: SIMBA YAFUNGUKIA ISHU YA PHIRI NA KUFUNGA