HUKO Yanga unapikwa mfumo mpya wa kuhakikisha kocha, Miguel Gamondi anatumia namba 10 wawili katika kikosi chake ili kuongeza ubunifu katika kufunga mabao yatakayoisaidia Yanga kuwa bora msimu huu.
Gamondi tayari ameshawafurahisha mashabiki wa timu hiyo licha ya kupoteza mechi yao dhidi ya Simba kwenye fainali ya Ngao ya Jamii ambapo kikosi chake kilionyesha
kiwango bora na kucheza soka la kasi na la kuvutia zaidi.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga kimeeleza juu ya mpango wa kocha Gamondi kutaka kuwatumia namba 10 wawili katika kikosi chake
wenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao ili kuongeza ubunifu katika kikosi chao.
“Yanga ya Gamondi kila mtu ameiona ni kwa jinsi gani ina uwezo mzuri wa kucheza soka la kushambulia kwa kasi na kuzuia pia kwa kasi kubwa,lakini tatizo kubwa ambalo limeonekana mpaka sasa ni kwenye suala la upatikanaji wa mabao imekuwa ni kama tatizo.
“Hivyo ili kulahisisha katika kazi ya kufunga jambo ambalo mwalimu Gamond analifanya ni kutengeneza mfumo ambao ataweza kuwatumia namba 10 wawili
wenye uwezo wa kufunga mabao kisha wakacheza katika kikosi kimoja.
“Kama ambavyo unafahamu kwa sasa Yanga kuna namba kumi watatu katika kikosi chetu ambao ni Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua. Maxi yeye huweza kucheza kama winga hivyo ni wazi jambo hili litawahusu
zaidi Pacome na Azizi Ki.”
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe yeye amesema kuwa, “Kuna kikosi ambacho mwalimu Gamondi
atakipanga siku na Yanga itakuwa inapata ushindi wa mabao mengi kuanzia mabao 9 na kuendelea, Yanga hii ya sasa ina wachezaji wazuri wenye uwezo wa kupambana ndani ya nchi na nje ya nchi,” amesema
kiongozi huyo.