Home Sports SUALA LA KITAYOSCE TUACHE KUPEPESA WAMEKOSEA

SUALA LA KITAYOSCE TUACHE KUPEPESA WAMEKOSEA

SAKATA la kwanza la Ligi Kuu Bara katika msimu mpya wa 2023/24 ni kuhusiana na suala la kuvunjika kwa mechi kati ya Azam FC dhidi ya Kitayose ya Tabora.

Mechi hiyo kwenye Uwanja wa Chamazi iliisha hata kabla ya mapumziko kutokana na wageni Kiyayose kuanza na wachezaji pungufu na baadaye wakapungua kutokana na kuumia kwa kipa na mchezaji mwingine.

Kitayose walianza wakiwa na wachezaji saba kwa kuwa walikuwa hawajakamilisha baadhi ya usajili wa wachezaji wake.

Hii ilitokana na usajili wao kuzuiliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo lilikuwa limewapa siku 45 baada ya kujirisha.

Fifa ilijirisha kuwa Kitayose kweli ilistahili kumlipa mchezaji wa kutoka Ghana. Lakini baada ya hapo ilionekana uongozi wa klabu hiyo ambayo imepanda ligi kuu msimu huu ulikuwa haujalichukulia suala kwa umakini mkubwa.

Wakati mwingine mamlaka kama Fifa huwa hazina utani katika masuala ya uchukuaji hatua. Lakini wengi hudhani mambo mengi ni siasa au utani kama ambavyo hufanya katika mamlaka zetu kama TFF.

Fifa walizuia usajili na hii maana yake ni lazima suala hilo lifanyiwe kazi na TFF tena. Mwisho ndio hiyo aibu kwa Kitayose kufungwa kwa mabao 4-0 lakini mpira umevunjika na hakika si jambo zuri.

Ajabu sana, unaona baadhi ya watu walianza kurusha shutuma kwa TFF na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa madai kwamba ilipaswa kuisaidia Kitayose kwa uzembe wao.

Mifano wanayotoa wakati mwingine unasema huenda wanazungumza mambo wasiyoyaelewa kama lile la Simba kuruhusiwa kutocheza mechi yake dhidi ya Kagera Sugar msimu mmoja umepita kutokana na wachezaji wake kutajwa wanaumwa mafua.

Wanaotoa mfano wamesahau kilikuwa ni kipindi cha Covid 19 na kilikuwa kipindi ambacho tahadhari ilikuwa inatakiwa kuchukuliwa kwa kiwango kikubwa sana.

Mfano mwingine umekuwa ni ule wa Yanga kuondoka uwanjani katika mechi ya watani wao wakifuata kanuni na Simba wakafuata barua ya kusogezwa muda wa mchezo na hii ikafanya mchezo usichezwe, jambo ambalo kiuhalisia unaona wanaotoa mfano, hawafikirii wanachokizungumza.

Yaani hawa Kitayose waliofanya uzembe, wakashindwa kulipa, walipopelekewa madai hawakutekeleza. Kesi ikaenda Fifa, lakini bado wakashindwa kufanya malipo hadi wanafungiwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitayose, Thabiti Kandoro ambaye ndiye alikuwa na siku nne kazini, amekiri kulikuwa na tatizo.

Kandoro amekuwa muungwana ameeleza namna ambavyo wameanza kulifanyia kazi jambo hilo na kukubali kweli walilipa siku ya mechi lakini suala la aliyepokea malipo alikuwa mzito kuandika email Fifa kuelezea kuwa amepokea.

Ukiangalia ni uzembe wa Kitayose na anayetaka wasaidiwe lakini hakuwashauri kuwa wangeomba kusaidiwa kwa kuwa ukimya wao ilionyesha wanajua namna ya kulimaliza suala hilo.

Achana na hivyo, hata kocha naye alihakikishiwa na uongozi kuwa atawatumia wachezaji wake wote hadi muda mchache kabla ya kwenda katika mechi.

Maana yake, Kitayose hawakuomba msaada kwa kuwa walikuwa wanajua watalimaliza suala hilo siku ya mambo yatakuwa mazuri. Sasa vipi TFF ingewasaidia tena siku ya mchezo?

Vizuri sana wakati mwingine tukajikita katika kushauri kwa kusema ukweli badala ya kupiga kelele tu ilimradi.

Inapendeza sana kama tunataka watu wajirekebishe, hata kama tunawapenda, basi tuwaeleze ukweli kutokana na jambo fulani.

Haiwezekani hata kidogo ukataka kumjenga mtu kwa kuona anachokosea ni sahihi na ukataka kuwavika wengine makosa yake ambayo yako wazi.

Kiuhalisia, kama Kitayose ni waungwana walipaswa kuwaomba radhi mashabiki wa soka wa Mkoa wa Tabora na Tanzania kwa ujumla kitendo ambacho hakikuwa cha kiungwana.

Mechi ilikuwa mubasharaa, soka la Tanzania linapewa heshima kubwa na kilichotokea hakipaswi kutokea.

Bahati mbaya timu iliyofanya ndio imepanda msimu na inaonekana haijajipanga au bado haikumbiki kuwa imeshapanda ligi kuu.

Kandoro ana kazi kubwa na lazima awe tayari kubadilisha mambo kama hayo yasitokee tena wakati mwingine.

Previous articleVIDEO: MORRISON KUISHTAKI YANGA FIFA/ TIMU ZIWALIPE WACHEZAJI
Next articleCHAMA NA LUIS NA JAMBO LINGINE