Home Sports MAUA YA MKWAKWANI YAMWAGIWE KIRUMBA, ALI HASSAN MWINYI

MAUA YA MKWAKWANI YAMWAGIWE KIRUMBA, ALI HASSAN MWINYI

WAKATI Uwanja wa Mkapa ukiwa katika matengenezo makubwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefanya juhudi kubwa kuhakikisha ratiba za mchezo wa soka katika ngazi ya juu kabisa zinaendelea.

Ratiba hizo ni zile za kuanza kwa msimu mpya wa 2023/24 na safari hii zilikuwa ni kuanzia mechi za Ngao ya Jamii.

Ngao hiyo safari hii ilibadilika, badala ya timu mbili kukutana katika mechi moja na kumaliza kazi, mambo yalikuwa yamebadilika baada ya TFF, Bodi ya Ligi na klabu kukubaliana.

Ikawa ni michuano mifupi ya timu zilizomaliza katika Top Four ya msimu uliopita ambayo ndio cream inayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa kupigia Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Hakuna ubishi, bila Dar es Salaam hakuna namna tena, hakuna ujanja kwa kuwa kila uwanja bora uko Dar es Salaam na vingine vinafuatia.

Kwanza ni Uwanja wa Mkapa, halafu Uwanja wa Uhuru, unamalizia na Uwanja wa Chamazi. Baada ya hapo unaweza kuangalia na viwanja vingine sasa?

Sasa kwa michuano mikubwa kama hiyo ungeipeleka wapi, kama nilivyosema TFF na wadau wake wakaifanya kazi yao kwa hesabu sahihi kabisa.

Marekebisho makubwa ya Uwanja wa Mkwakwani ambao sehemu ya kuchezea lilikuwa tatizo kubwa sana kama vilivyo viwanja vingine nje ya Dar es Salaam ukiachana na vichache vyenye nyasi bandia.

Umerekebishwa na hata kama hauna kiwango cha Uwanja wa Mkapa lakini tumeona, mechi za timu zote nne zimechezwa na hakukuwa na shida.

Kiwango ambacho Mkwakwani hatujawahi kuiona na ilikuwa kama inaonekana haiwezekani kuwa hivyo.

Awali iliwahi kufanyika lakini haikufikia hapo na mambo sasa yamewezekana na hili tuamini kumbe ni jambo linalowezekana kama wahusika wakiamua.

Achana na suala la pitch tu, angalia taa. Leo hakuna hofu kuona mechi inaanza kuchezwa saa 1 usiku. Mkwakwani ni kama Ulaya vile.

Sote tunajua wakazi wa Tanga wanapenda sana mpira, leo wanapata nafasi hii ya kuutumia uwanja huo usiku na hakuna ubishi tena inawezekana kwa kuwa mechi zimechezwa hapo.

Kutakuwa na mapungufu kadhaa kutokana na uwanja kuwa ni wa kizamani lakini kama maboresho au marekebisho yataendelea, basi itafanikiwa na ubora utafikiwa.

Huu ndio wakati wa kujiuliza sasa na kupata jibu katika maswali ambayo tumekuwa tukijiuliza kwa muda mrefu sana hasa wale tunaopenda maendeleo ya michezo.

Vipi mikoani viwanja viwe na viwango duni? Kwanini imekuwa haiwezekani? Chama cha Mapinduzi (CCM) ni wamiliki, wamekuwa hawafanyi hayo marekebisho na ndio wenye viwanja! Nani aanzishe kurekebisha baadhi ya viwanja vya mikoani viwe bora zaidi.

Tuna viwanja vingi vizuri kama Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Kambarage mkoani Shinyanga au Sokoine, Mbeya, Jamhuri mkoani Morogoro.

TFF waliwaingia vipi CCM hadi wakakubali kuhusiana na Mkwawani? Kwanini wasifanye hivyo kwa viwanja hivyo vinginena kuifanya Tanzania iwe tofauti kabisa.

Hatuwezi kuendesha mpira kwa mafanikio kwa kutegemea viwanja vya Dar es Salaam peke yake. Tutakuwa tunategemea kidole kimoja kuendesha mwili mzima.

Ingawa imekuja kama dharura lakini inaweza kutumika kama kipimo cha kuangalia kuwa lililotokea linawezekana na kwingine pia.

Uzuri wa hivi viwanja, mpira unapochezwa inakuwa ni kwa kila timu. Timu za Dar es Salaam pia zinacheza katika mikoa mingine kama ambavyo zinafanya timu za Mbeya, Mwanza, Dodoma, Shinyanga, Tabora, Iringa, Ruvuma, Arusha na kwingineko.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametuambia kuwa Serikali yake itajenga viwanja Arusha na Dodoma. Huko tuiachie serikali na badala yake, tuwapa nguvu na kuwanja mkono TFF kuingia katika maeneo mengine kufanya maboresho zaidi.

Previous articleKINAWAKA LEO LIGI KUU BARA
Next articleIHEFU YAANZA KWA KUPOTEZA LIGI KUU BARA, GEITA KICHEKO