“TUNA mikataba na bado tunahangaika. Suala la Clatous Chama limeniacha hoi. Mikataba ni kama vile haina maana Bongo. How? Tumeambiwa Chama ataenda Uturuki. Safi. Amesaini mkataba mpya? Hapana, kumbe alikuwa na mkataba.
“Alitaka kuboreshewa maslahi yake. Walikuwa na makubaliano ya mdomo au katika vipengele vya mkataba? Kama kuna kiongozi mmoja alikuwa kando anavuta fegi akamwambia kwa mdomo ‘mwisho wa msimu tutaboresha maslahi’. Haya maneno yapo katika mkataba?
“Kama hayapo hayatambuliki. Kwa akili yake nzuri alikubalije kwa maneno jambo hili? Kwanini lisiwe katika mkataba na kwa kiasi gani? Tunasumbua mashabiki na wanachama wakati dunia ya leo kila kitu inabidi kiwe wazi.
“Wakati mwingine mchezaji anajiona muhimu na anaichukua timu kama mateka. Kila hitaji lake kwanini lisiwe kwa mujibu wa mkataba?
“Nataka niwe upande wa viongozi na klabu. Sidhani kama walikuwa na wehu wa kutoboresha maslahi yake kama kweli kulikuwa na vipengele hivi. Hasa kwa kuzingatia umuhimu wake. Kwanini mashabiki wabaki gizani wanatazama nyota nyota wakati mikataba ipo? Sijui nimeeleweka?” alimaliza kueleza mchambuzi nguli wa michezo nchini Edo Kumwembe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
Kwa takribani wiki kulikuwa na sintofahamu kubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba kuhusiana na na kiungo mshambuliaji wao Chama hasa baada ya nyota huyo kutosafiri na timu kwenda Uturuki kutokana na changamoto baina yake na mabosi wa Simba.
Kama ambavyo Edo Kumwembe hapo juu amelielezea, inadaiwa kuwa Chama aligoma kusafiri na wenzake kwa kudaiwa kuwa alikuwa akiushinikiza uongozi wa Simba kufanya maboresho ya maslahi yake.
Baada ya sintofahamu kuwa kubwa kiasi cha kuanza kumhusisha staa huyo na watani zao wa Jadi Yanga, mtego huo uliisha na Simba kutoa taarifa ifuatayo: “Baada ya majadiliano na uongozi kumalizika vizuri kiungo mshambuliaji, Clatous Chama ataondoka nchini muda wowote kutoka sasa kuelekea Uturuki kujiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu.
“Chama ataondoka pamoja na kiungo mkabaji, Fabrice Ngoma ambaye mchakato wa kupata vibali vya kuingia Uturuki unaendelea vizuri. Wawili hao wakifika Uturuki ina maanisha wachezaji wote tuliowasajili kwa ajili ya msimu ujao watakuwa wamekamilika, ukiacha wale ambao bado hatujawatangaza.”
Ikumbukwe suala hili si mara ya kwanza kuibuka hapa nchini tena kwa mchezaji huyohuyo, lakini pia ni juzi tu tumetoka kumalizana na sakata zito la aliyekiwa kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na timu yake hiyo ya zamani kiasi cha nguvu ya dola kutumika kulimaliza.
Kujirudia kwa mitifuano hii ya kimkataba inaturudisha kwenye ile kauli mbiu ya soka letu kivyetu vyetu. Nadhani inabidi ifike wakati sasa tunapaswa kubadilika na kuendana na kasi ya ukuaji tunaojivunia wa soka letu.
Tunasema ligi yetu imekua sana, kwamba ipo nafasi ya 5 Afrika, ni jambo la kujivunia lakini tusiishie kwenye ligi pekee bali mifumo yote ya uendeshaji wakiwemo viongozi na wachezaji wakue na kuacha mambo ya kitoto, hususani linapokuja suala la mikataba.