SIMBA YAMFUATA MWAMBA HUYU

KLABU ya Simba imerudi tena ndani ya klabu ya Cotton Sports FC ya nchini Cameroon kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa kati Che Fondoh Molane.

Beki huyo ni kati ya wachezaji waliokuwa katika mipango ya kusajiliwa na Simba katika msimu huu katika kuiboresha safu ya ulinzi.

Simba hivi karibuni ilitangaza kuachana na beki wa kati Muivory Coast, Mohammed Outtara ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango bora msimu huu.

Mmoja wa mabosi wa Simba, amesema kuwa baada ya kukataliwa ofa yao waliyowekewa mezani Cotton Sports ambayo ni dola 65,000 sasa wanajipanga kwa ajili ya kupeleka ofa ya dola 100,000 (Shilingi milioni 239.6 za Kitanzania) ili kuipata saini ya mchezaji huyo.

Aliongeza kuwa beki huyo mwenyewe amekubali kujiunga na Simba, licha ya ugumu wanaoupata katika klabu yake hiyo.

“Ni lazima tumpate Che Molane ambaye tunaamini atakuja kuiboresha vyema safu yetu ya ulinzi katika msimu ujao.

“Beki tumepanga kumsajili kutokana na uzoefu wake wa kucheza michuano ya kimataifa, hivyo kwa kusaidiana na Inonga (Hennock) ninaamini tutakuwa vizuri.

“Ugumu wa kumpata beki huyo tunaupata kutoka kwa klabu yake ya Cotton Sports yenye mkataba naye, hivyo ni lazima tuuvunje,” alisema bosi huyo.

Akizungumza hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alizungumzia hilo la usajili kwa kusema kuwa: “Kila mchezaji aliyependekezwa na benchi la ufundi lazima asajiliwe, hivyo Wanasimba waondoe hofu.”