NTIBANZOKIZA NA TUZO MKONONI, MABAO SABABU

MKONONI ana tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi Mei baada ya kuwashinda nyota wawili alioingia nao fainali.

Nyota huyo ni shuhuda wa watani zao wa jadi Yanga wakisepa na taji la ligi kwa msimu wa 2022/23 wakiwa na tofauti ya pointi tano.

Anaitwa Saido Ntibanzokiza kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye alitupia mabao 7 ndani ya mwezi Mei.

Alifunga mabao matano kwenye mchezo mmoja dhidi ya Polisi Tanzania na alifunga mawili mchezo dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Uhuru.

Ni Prince Dube wa Azam na Charlse Ilanfya wa Mtibwa Sugar waliingia pamoja kwenye fainali kuwania tuzo hiyo.

Jumla Ntbanzokiza ametupia mabao 17 sawa na mshikaji wake Fiston Mayele mali ya Yanga.

Tuzo ya mfungaji bora itajulikana leo nani atasepa nayo baada ya kamati kuja na majibu waliyokaa kwenye kikao chao.

Kwa upande wa kocha bora mwezi Mei ni Roberto Oliveira mali ya Simba.