SIMBA: NTIBANZOKIZA ATAKUWA MFUNGAJI BORA

BOSI wa Simba kwenye idara ya Habari na Mawasiliano akiwa Ahmed Ally ameweka wazi kuwa suala lililobaki kwa sasa ni timu nzima kumsaidia Saido Ntibanzokiza kuwa mfungaji bora.

Nyota huyo ametupia mabao 15 kwenye ligi ameachwa kwa bao moja na mfungaji namba moja Fiston Mayele ambaye yupo ndani ya Yanga akiwa na mabao 16.

Leo Yanga itamenyana na Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya na Simba dhidi ya Coastal Union.

Meneja wa Idara ya Habari Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kwa sasa suala la tuzo ya ufungaji bora hilo linakwenda kuwa ni la timu nzima itafanikisha jambo hilo.

“Tunahitaji kiatu cha ufungaji bora na inawezekana hasa ukiangalia kwamba Ntibanzokiza takwimu zinambeba, kafunga mabao matano ikiwa ni rekodi kubwa msimu huu kwa mchezaji mmoja.

“Katika mabao hayo matano amepewa pasi na John Bocco aliyekuwa kwenye nafasi ya kufunga na bao moja Kibu Dennis alikuwa na nafasi ya kufunga lakini hakufunga hivyo tutamsaidia kutwaa tuzo ya ufungaji bora.

“Mchezo wetu dhidi ya Coastal Union tuna amini atafunga kwani ni mabao mawili ambayo yamebaki na rekodi zinambeba kutokana na uwezo wake,” amesema Ally.