YANGA HAWAJARIDHIKA KABISA NA WALICHOPATA KIMATAIFA

NASREDDINE Nabi Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa hawajaridhika na kuongoza kundi katika hatua ya Kombe la Shirikisho Afrika bali wanahitaji kusonga mbele mpaka hatua ya nusu fainali.

Yanga inayonolewa na raia huyo wa Tunissia ilitinga hatua ya robo fainali ikiwa na pointi 13 katika kundi D na kete yake ya kwanza robo fainali ya kwanza ni dhidi ya Rivers United ugenini.

Baada ya dakika 90 ilikuwa Rivers United 0-2 Yanga huku mtupiaji akiwa ni mshambuliaji Fiston Mayele akitumia pasi za Bakari Mwamnyeto ambaye ni nahodha ilikuwa dakika ya 71 na 82.

Kocha huyo ameweka wazi kuwa kila mchezaji anatambua namna walivyopoteza dhidi ya timu hiyo mwaka 2021 sababu wanazitambua na wamezifanyia kazi.

“Tunatambua wapinzani wetu Rivers United sio timu mbaya na rekodi ya kupoteza mbele yao 2021 tunakumbuka hivyo kwenye mechi zote tutapambana kupata ushindi wa jumla ili kusonga mbele kwenye hatua hii ya kimataifa.

“Kuongoza kundi kwetu ni mafanikio lakini hatujaridhika kuishia hapo lazima tupambane kusonga mbele zaidi na inawezekana kwani timu yetu imebadilika na wachezaji wanajuhudi,”.

Leo Aprili 24 msafara wa Yanga umeanza safari kutoka Nigeria ambapo utapitia Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kuibukia Bongo.