ALLY Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa kupoteza mchezo wao dhidi ya Simba sio mwisho wa kazi maisha lazima yaendelee.
Kabla ya mchezo Aprili 16 Kamwe alimwambia Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba Ahmed Ally kuwa wiki ya Jumatatu ya Aprili 17/2023 itakuwa ni ya masimango kwa mmoja huku mwingine akiwa na furaha.
Katika mazungumzo yao Ally alibainisha kuwa wao, (Simba) hawana huzuni bali ni sherehe tupu.
Baada ya mchezo Yanga ilishuhudia ubao ukisoma Simba 2-0 Yanga na kuziacha pointi tatu mazima Uwanja wa Mkapa.
Kamwe amesema:”Mashabiki wa Yanga wanatambua hali halisi ilivyo na wamepokea matokea kwa aina ya kipekee kamaingekuwa ni wengine wangeanza kelele za kocha atuachie timu yetu.
“Kwa kilichotokea maisha lazima yaendelee na wachezaji wanatambua namna mashabiki walivyopata maumivu, bado kuna mechi zinakuja tunaamini tutafanya kazi kubwa,” amesema.
Yanga ni vinara kwenye ligi wakiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 26 huku Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi 63.